Amir Mhando |
Na Princess Asia
KAMATI ya
Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA),
iliyokutana katikati ya wiki jijini Dar es Salaam imekubaliana na mapendekezo
ya baadhi ya wanachama kuomba isogeze mbele kwa wiki moja Mkutano Mkuu wa chama
hicho.
Katibu wa
TASWA, Amir Mhando ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, awali mkutano huo
ulipangwa kufanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel,
Bagamoyo mkoani Pwani, lakini sasa utafanyika Desemba 28 na 29 mahali hapo
hapo.
Amesema hatua
hiyo ya kusogeza mbele inatokana na baadhi ya wanachama kuomba iwe hivyo kutokana
na Jumamosi ya Desemba 22 kutakuwa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya
timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ile ya Zambia ‘Chipolopolo’
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Amesema kwa
msingi huo wamekubaliana na hoja kwamba mchezo huo kwa kiasi fulani ungeathiri
umakini wa wajumbe kwenye mkutano kwa namna moja au nyingine, hivyo kupunguza
tija.
Amesema wanaamini
idadi kubwa ya wanachama waliothibitisha kushiriki ni ishara kwamba wengi
wanataka kujumuika kwa asilimia kubwa katika kukijenga chama chao, hivyo
hatuoni sababu ya kufanya mkutano kwa kukurupuka.
Alisema hadi
kufikia Desemba 15 ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya wanachama kuthibitisha
ushiriki wa mkutano zaidi ya asilimia 95 ya wanachama walikuwa wamethibitisha
kushiriki.
“Kutokana na
hali hiyo wote waliothibitisha ushiriki huo na ni hai watajulishwa kwa barua
rasmi, ambazo zitaeleza utaratibu wa namna ya kufika Bagamoyo na mambo mengine
muhimu yatakavyokuwa,”.
“Barua
zitaanza kutoka wakati wowote kuanzia Jumatano ijayo baada ya kikao cha Kamati
ya Utendaji ya TASWA kinachotarajiwa kufanyika siku hiyo,”.
Mhando amesema
pia tayari TASWA imewaalika wadau mbalimbali wakiwemo wahariri wakongwe ambao
wamethibitisha kushiriki kwenye mkutano huo wa aina yake. Amesema TASWA baada
ya kupata udhamini wa Zantel kwa ajili
ya mkutano huo bado inaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali na
inatarajia kuwatangaza wakati wowote mambo yatakavyokuwa mazuri.
Wakati huo
huo: Mhando amesema kwamba TASWA, inawapongeza viongozi wapya wa Kamati ya
Olimpiki Tanzania (TOC) walioingia madarakani Desemba 8, mwaka huu mkoani
Dodoma, ambapo Ghullam Rashid alichaguliwa tena kuwa Rais, huku Filbert Bayi
akichaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu.
Alisema wanaahidi
kuendeleza kushirikiana na uongozi wa TOC kama ilivyokuwa wakati uliopita na
kuwatakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yao na tuna imani watafanya
vyema.
Aidha,
Mhando amesema TASWA imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa
mwandishi wa zamani wa habari za michezo, Amina Singo kilichotokea usiku wa
kuamkia leo.
“Tunaungana
na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu kwani wakati wa uhai wake
alikuwa mdau mkubwa wa TASWA wakati huo akiwa mtangazaji wa habari za michezo
wa Redio Times FM, hivyo kifo chake ni pengo kubwa kwa tasnia ya uandishi wa
habari hapa nchini,”alisema.
Kwa mujibu
wa marafiki za marehemu msiba upo Mbezi na mipango ya mazishi inaendelea.