Umony |
Na Prince Akbar
MCHEZAJI
bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, Brian
Umony anatarajiwa kuwasili leo mjini Dar es Salaam kujiunga na klabu yake mpya,
Azam FC.
Umony anawasili
siku mbili tu, baada ya wachezaji wengine wapya wa Azam, kutoka Kenya, beki
Joackins Atudo na kiungo Humphrey Mieno kuwasili Dar es Salaam kujiunga na
klabu yao hiyo mpya.
Nyota hao
wote watatu, watakuwemo kwenye kikosi kitakachokwenda visiwani Zanzibar kesho kwenye
michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Brian
amerejea nyumbani Uganda mwaka huu na kujiunga na KCC baada ya kumaliza mkataba
wake katika klabu ya Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
Mwaka 2009, ilikuwa
aje kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, lakini Wekundu hao wa Msimbazi wakazidiwa
kete na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Umony
aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya
Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa
mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C. kabla ya kurejea Uganda na
sasa anakuja kuanza maisha mapya Azam FC 2012.
Kwa upande
wa Atudo na Mieno, wao walianza kuichezea Azam katikati ya mwezi huu na
walikuwepo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichotwaa Kombe la Hisani la Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la
DRC wiki iliyopita, baada ya kuwachapa wenyeji, Dragons FC kwa penalti 4-2
kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Azam iliingia
fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya DRC
Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
Kikosi kizima
cha Azam kilichoshiriki mashindano hayo ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre
Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki,
Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson
Kakolaki, Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri
Salum, Humphrey Mieno na Joackins Atudo.
Katika
mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake
matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti. Mchezaji mwingine wa kigeni wa
Azam, Brian Umony wa Uganda, atajiunga na timu hiyo baada ya sikukuu pia.
Azam
wamepangwa Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro,
Coastal Union ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Kundi A lina
timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Michuano ya Kombe
la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya
Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka
ndani na nje ya Tanzania.