Azam Academy wakiwa katika picha ya pamoja na Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Pele wa Ghana alipowatembelea miezi miwili iliyopita Azam Complex, Dar es Salaam |
Na Prince Akbar
TIMU sita
zimeshakata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la
Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 (U20) wa klabu za
Ligi Kuu ya Tanzania.
Hatua ya
robo fainali ya michuano hiyo inayofanyika viwanja vya Karume na Chamazi, Dar
es Salaam na kudhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitai maji Uhai
itafanyika Desemba 19 mwaka huu kwenye viwanja hivyo hivyo.
Timu
zilizofuzu kutoka kundi A ni Coastal
Union ya Tanga, Mtibwa Sugar ya Morogoro na JKT Ruvu ya Dar es Salaam. Kundi C
ni Oljoro JKT ya Arusha na Ruvu Shooting ya Pwani wakati iliyofuzu kutoka kundi
A hadi sasa ni Azam pekee.
Katika mechi
zilizochezwa leo asubuhi (Desemba 17 mwaka huu) Coastal Union na Mtibwa Sugar
zimetoka suluhu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, wakati Uwanja wa Azam
ulishuhudia African Lyon ikiifunga Mgambo Shooting mabao 2-1.
Nafasi mbili
za robo fainali zilizobaki kutoka kundi B zinawaniwa na timu za Simba, African
Lyon na Polisi Morogoro. Mechi itakayochezwa leo saa 10 jioni katika Uwanja wa
Chamazi kati ya Polisi Morogoro na Simba ndiyo itakayoamua timu zitakazoungana
na Azam kutoka kundi hilo.