Kikosi cha Zambia kilichotwaa ubingwa wa Afrika mapema mwaka huu |
Na Prince Akbar
MABINGWA wa
Afrika, Zambia ‘Chipolopolo’ wakiwa na msafara wa watu 32 wanatarajiwa kuwasili
nchini leo tayari kwa mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Tanzania, Taifa Stars.
Timu hiyo
itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 kamili
jioni kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Lusaka.
Mbali ya
wachezaji 24, msafara wa Zambia ambayo inakuja nchini kwa ajili ya mechi dhidi
ya Taifa Stars utakuwa na maofisa wengine wanane wakiwemo wa benchi la ufundi
linaloongozwa na Kocha Herve Renard aliyeipa timu hiyo ubingwa wa Afrika mwaka
jana nchini Gabon.
Wachezaji
kwenye msafara huo ni Chintu Kampamba, Chisamba Lungu, Christopher Katongo,
Danny Munyau, Davy Kaumbwa, Derrick Mwansa, Evans Kangwa, Felix Katongo na
Francis Kasonde.
Given
Singuluma, Hichani Himonde, Isaac Chansa, James Chamanga, Jimmy Chisenga, Jonas
Sakuwaha, Joshua Titima, Kalililo Kakonje, Moses Phiri, Mukuka Mulenga,
Rainford Kalaba, Rodrick Kabwe, Salulani Phiri, Shadrack Malambo na Stoppila
Sunzu.
Mechi dhidi
ya Taifa Stars itafanyika Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Dar es Salaam tangu Desemba 12
mwaka huu chini ya Kocha Kim Poulsen kujiandaa kwa mechi hiyo.
Viingilio
katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh.
7,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B
wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Tiketi
zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mechi katika vituo vya Shule ya
Sekondari Benjamin Mkapa, Uwanja wa Uhuru, Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa
Ohio na Samora, Sokoni Kariakoo, kituo cha mafuta cha Ubungo OilCom na Dar Live
Mbagala.
Pia tiketi
zitauzwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu) kwenye tamasha la Kilimanjaro Premium
Lager kuhamasisha washabiki wa Taifa Stars litakalofanyika kwenye viwanja vya
Sigara, Chang’ombe.