Kikosi cha Azam kilichokuwa tishio DRC |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
MABINGWA wa
Kombe la Hisani, linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Azam FC ya Dar es Salaam wanaondoka leo saa 5:00
za hapa, sawa na saa 7:00 mchana za Afrika Mashariki, kurejea nyumbani Tanzania
kwa furaha baada ya kutwaa taji hilo.
Azam
wanaondoka kwa ndege ya Kenya Airwarys na watapitia Nairobi, ambako
wataunganisha ndege ya kurejea Dar es Salaam.
Katibu wa
Azam, Nassor Idrisa amesema kwamba timu ikirejea Dar es Salaam, wachezaji
watapewa mapumziko ya siku mbili kwa ajili ya sikukuu ya Krisimasi na baada ya
hapo watakutana kujiandaa kwa safari ya Zanzibar kwenda kutetea Kombe lao la
Mapinduzi.
Azam juzi ilitwaa
ubingwa wa Kombe la Hisani baada ya kuwafunga wenyeji, Dragons FC kwa penalti
4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs mjini
hapa.
Azam
walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha
dakika ya 75 na katika mikwaju ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili
ya Dragons, wakati Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji
Nuhu walifunga penalti za Azam.
Azam juzi ilicheza
bila kocha wake Mkuu, Muingereza Stewart Hall ambaye aliondoka juzi usiku mjini
hapa kwenda kwao Uingereza kwa ajili ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya na
iliongozwa na Kocha Msaidizi, Kali Ongala.
Azam iliingia
fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya hapa
Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
Kikosi cha
Azam kilichoshiriki mashindano haya ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre
Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki,
Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson Kakolaki,
Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri Salum, Humphrey
Mieno na Joackins Atudo.
Katika
mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake
matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti.