Umony |
Na Princess Asia
MCHEZAJI
bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Kagame,
Brian Umony ‘dizaini’ ameanza kuwafanyia ‘mizinguo’ Azam FC kutokana na
kushindwa kuwasili jana mjini Dar es Salaam kujiunga na klabu yake hiyo mpya
kama alivyoahidi.
Habari
kutoka Azam, zimesema kutwa nzima ya jana Umony alikuwa hapatikani kwenye simu,
lakini baafaye akatuma barua pepe atafika saa tano, hakusema ya lini.
Wakati Umony
analeta mizinguo, wachezaji wengine wapya wa Azam, kutoka Kenya, beki Joackins
Atudo na kiungo Humphrey Mieno wamekwishawasili Dar es Salaam kujiunga na klabu
yao hiyo mpya.
Nyota hao,
watakuwemo kwenye kikosi kitakachokwenda visiwani Zanzibar kesho kwenye
michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Brian
amerejea nyumbani Uganda mwaka huu na kujiunga na KCC baada ya kumaliza mkataba
wake katika klabu ya Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
Mwaka 2009,
ilikuwa aje kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, lakini Wekundu hao wa Msimbazi
wakazidiwa kete na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Umony
aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya
Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa
mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C. kabla ya kurejea Uganda na
sasa anakuja kuanza maisha mapya Azam FC 2012.
Kwa upande
wa Atudo na Mieno, wao walianza kuichezea Azam katikati ya mwezi huu na walikuwepo
kwenye kikosi cha timu hiyo kilichotwaa Kombe la Hisani la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la
DRC wiki iliyopita, baada ya kuwachapa wenyeji, Dragons FC kwa penalti 4-2
kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Azam
iliingia fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark
FC ya DRC Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa
Martyrs.
Kikosi kizima
cha Azam kilichoshiriki mashindano hayo ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre
Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki,
Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson
Kakolaki, Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri
Salum, Humphrey Mieno na Joackins Atudo.
Katika
mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake
matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti. Mchezaji mwingine wa kigeni wa
Azam, Brian Umony wa Uganda, atajiunga na timu hiyo baada ya sikukuu pia.
Azam
wamepangwa Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro,
Coastal Union ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Kundi A lina
timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Michuano ya Kombe
la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya
Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka
ndani na nje ya Tanzania.