Na Prince Akbar
MICHUANO ya
Kombe la Uhai, inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo kadhaa, ukwemo kati ya
Mtibwa Sugar ya Morogoro dhidi ya Toto Africans ya Mwanza asubuhi kwenye Uwanja
wa Karume, Dar es Salaam.
Mechi
nyingine, Coastal Union ya Tanga itamenyana na JKT Ruvu ya Pwani mchana Uwanja
wa Karume, Oljoro JKT na Yanga asubuhi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Ruvu
Shooting ya Pwani na Kagera Sugar ya Bukoba mchana Chamazi, Mgambo Shooting ya
Tanga na Simba ya Dar es Salaam asubuhi Chamazi na African Lyon dhidi ya Azam
jioni Chamazi.
Katika mechi
za juzi, Coastal Union iliendelea kufanya vizuri kwenye michuano hiyo inayoshirikisha
wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya
kuifunga Toto Africans mabao 3-1.
Mabao ya Coastal
katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Chamazi yalifungwa na
Mohamed Miraji dakika ya 44, Abdul Banda (dk. ya 62) na Ramadhan Shame (dk. ya
83). Toto Africans ndiyo iliyoanza kupata bao dakika ya 30 lililofungwa na
Severin Constantine.
Coastal
Union ilishinda mechi yake ya kwanza mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika
michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji
Uhai.
Nayo Simba
iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon katika mechi ya kundi B
iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 12 mwaka huu) Uwanja wa Karume. Miraji Athuman
na Ramadhan Mzee ndiyo walioifungia Simba dakika ya 15 na 47 wakati la African
Lyon lilifungwa dakika ya 57 na Mbela Kashakala.
Polisi
Morogoro iliifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume wakati katika Uwanja wa
Azam, JKT Ruvu iliifunga Tanzania Prisons bao 1-0 lililofungwa dakika ya 16 na
Jacob Mambia. Yanga na Ruvu Shooting zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Chamazi.
Katika mechi
iliyochezwa jana asubuhi Uwanja wa Karume, Oljoro JKT iliizamisha Kagera Sugar
mabao 3-0, mabao ya Hamisi Saleh dakika ya 49 huku Shamir Mohamed akipachika
mawili dakika ya 52 na 55.