Waziri akisaidiwa na makipa wa timu yake kutoka uwanjani baada ya mechi juzi. Kulia Jackson Wandwi na kushoto Mwadini Ally |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
KIUNGO
Waziri Salum wa Azam FC, atakuwa nje ya Uwanja kwa wiki mbili kufuatia kuumia
katika mchezo wa juzi dhidi ya Real de Kinshasa kwenye Uwanja wa Martyrs mjini
hapa.
Daktari wa
Azam FC, Mjerumani Paulo Gomez ameiambia BIN ZUBEIRY jana mjini hapa kwamba Waziri
ameumia mfupa wa pembeni wa paja la kushoto na kwa sababu hiyo atakuwa nje kwa
muda wiki mbili akipata matibabu.
Kocha
Muingereza Stewart Hall amepokea kwa masikitiko taarifa hizo, akisema Waziri ni
mchezaji ambaye anainukia vizuri Azam na kumkosa katika mashindano haya
litakuwa pigo kwake.
Hata hivyo,
Stewart alisema atatumia wachezaji wengine wakati akimsubiri kiungo huyo
Mzanzibari apate ahueni.
Waziri
amecheza mechi zote tatu za Azam katika mashindano haya hadi juzi alipoumia
dakika ya 43 na kutoka nje.
Kiungo huyo
amekuwa akionyesha soka maridadi katika mashindano haya na kuashiria kwamba
ataibeba Azam katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho
mwakani.
Wachezaji
wengine majeruhi Azam ni kiungo Mzanzibari pia, Abdulhalim Humud anayesumbuliwa
na maumivu ya nyama za paja na mshambuliaji John Bocco, ambao wamebaki Dar es
Salaam.