Kim Poulsen |
Na Prince Akbar
MAKOCHA wa
Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen na Zambia (Chipolopolo) watakuwa na mkutano
na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Desemba 21 mwaka huu) kuzungumzia
pambano lao litakalochezwa Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Mkutano huo
utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF). Makocha hao watazungumzia maandalizi yao ya mwisho kabla
ya pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Sylvester Kirwa kuanzia saa 10
kamili jioni.
Pia makocha
hao watajibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu pambano hilo
litakalokutanisha timu hizo ambazo zimefanya vizuri kwenye orodha ya viwango
vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) vilivyotolewa
jana (Desemba 19 mwaka huu).
Wakati
Zambia ambao ni mabingwa wa Afrika wamepanda juu kwa viwango vya ubora kwa
nafasi nne, Taifa Stars ambayo katika mchezo uliopita iliifunga Kenya (Harambee
Stars) bao 1-0 imepanda kwa nafasi nne.
Taifa Stars
ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini tangu Desemba 12
mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo kubwa ya kirafiki inayotarajiwa kuwa ya
kuvutia.