Kikosi cha Uganda, Okwi wa kwanza kulia waliosimama na Kiiza ameinama mbele yake |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
ROBO Fainali
za mwisho za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge zinatarajiwa kupigwa leo kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole
mjini hapa.
Kenya, mabingwa
mara tano wa Kombe hilo katika miaka ya 1975, 1981, 1982, 1983 na 2002,
watamenyana na Malawi walioalikwa tu kuongeza changamoto ya mashindano kuanzia
saa 10:00 jioni.
Wenyeji,
mabingwa watetezi na mabingwa wa kihistoria wa mashindano haya, Uganda The
Cranes waliotwaa Kombe hilo katika miaka ya 1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992,
1996, 2000, 2003, 2008, 2009 na 2011, watamenyana na Ethiopia.
Ethiopia ni
timu pekee kati ya wanachama wa CECAFA, iliyofuzu kucheza Fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Afrika Kusini.
Mchezo kati
ya Kenya na Malawi unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua hata kama mashabiki
hawatakuwa wengi uwanjani.
Kenya na
Malawi ni vigumu kuutabiri kulingana na viwango vilivyoonyeshwa na timu zote
katika mashindano haya kutopishana sana.
Lakini Uganda
wanapewa nafasi kubwa ya kuwafunga Ethiopia, ambao katika michuano hii
hawajaonyesha kiwango cha kutisha kama ilivyo kawaida yao licha ya kufuzu
AFCON.
Brian Umony,
Hamisi Kiiza, Rpbert Ssentongo na Emmanuel Okwi- hizi zinatarajiwa kuwa silaha
za Korongo wa Kampala katika mchezo wa leo, lakini pia yupo kiungo mmoja hodari
sana Joseph Oyola.
Katika Robo
Fainali za kwanza jana Uwanja wa Lugogo, Zanzibar iliichapa Burundi kwa penalti
6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90. Kwa matokeo hayo, Zanzibar
sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
Shujaa wa
Zanzibar jana alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya
kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha wa
timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa
Burundin walipoteza penalti zao jana.
Ndikumana
alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya
lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo,
Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
Upande wa
Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya
Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu,
kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa
Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na
Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.
Mapema
katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali, Bara ilifanikiwa pia kuingia Nusu
baada ya kuilaza Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Lugogo mjini hapa.
Hadi
mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri
Kiemba, dakika mya 33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza
wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John
Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na
aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
Katika hicho
kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya
Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19
Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars pamoja
na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri
ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha
na ikawapita wote.
Ngassa tena,
katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda
nje sentimita chache.
Kipindi cha
pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na
Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
Hata hivyo,
walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili dakika ya 53 baada ya
John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti
kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.