Wakili Mgongolwa |
Na Mahmoud Zubeiry
KAMATI ya
Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini
ya Mwenyekiti wake, Wakili Alex Mgongolwa, inatarajiwa kukutana kesho mjini Dar
es Salaam kujadili uhalali wa kuuzwa kwa mchezaji Mrisho Ngassa.
Ofisa Habari
wa TFF, Boniphace Wambura Mgoyo amesema mchana wa leo katika Mkutano na Waandishi
wa Habari kwamba, Kamati hiyo inakutana kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na
klabu ya Simba iliyokuwa inamtumia mchezaji huyo kwa mkopo kutoka Azam FC.
Hata hivyo,
Kamati hiyo itakutana huku kukiwa kuna taarifa kwamba, Simba SC na Azam FC
zimefikia makubaliano ya kumuuza kwa pamoja mshambuliaji huyo kwenda El
Merreikh ya Sudan.
Habari za
ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwenye kikao cha pamoja kati ya
Simba na Azam jana, zimesema kwamba Merreikh imeongeza dau la kumnunua Ngassa
kutoka dola za Kimarekani 70,000 hadi 100,000, zaidi ya Sh. Milioni 150 za
Tanzania.
Baada ya
kuongeza dau hilo, Azam ilikutana na Simba kujadili pamoja ofa hiyo mpya na
kukubaliana kumuuza na kugawana nusu kwa nusu.
Upande wa
Azam uliwakilishwa na mmoja wa Wakurugenzi wa bodi ya klabu hiyo, wakati kwa
Simba waliwakilishwa na Makamu wao Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
Upande wa
maslahi ya mchezaji umeboreshwa pia, Ngassa sasa atapewa dola za Kimarekani 75,000
zaidi ya Sh. Milioni 120,000 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na mshahara
utabaki kuwa dola 4,000 (Sh. Milioni 6).
Habari
zinasema kwamba, baada ya makubaliano hayo, leo Simba na Azam watasaini mkataba
na Azam na kumuuza rasmi mchezaji huyo.
Hata hivyo,
tangu wakati kikao hicho kinaendelea jioni ya jana, Ngassa alikuwa akitafutwa
ili kuhusishwa, lakini hakupatikana kwenye simu.
Wasiwasi
umeibuka kwamba huenda Ngassa anaweza akawa ameghairi mpango wa kwenda Merreikh
kutokana na ushauri mbaya wa watu wake wa karibu. Mchezaji mmoja wa timu ya
taifa, aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba Ngassa anafikiria kuachana na mpango wa
kucheza Sudan, kwa sababu anasikia ni nchi ya Kiislamu na haina starehe.
Wapembuzi wa
mambo wanasema kwamba, ilipofikia Ngassa anahitaji ushauri nasaha, kwani nafasi
aliyopata ni adimu na ni muhimu kwa taifa na hata kwa maslahi yake binafsi.
Achilia
mbali maslahi mazuri, lakini anakwenda kucheza timu ya ushindani ambayo itakuza
kiwango chake aweze kuisaidia timu ya taifa pia. Merreikh ni timu ambayo karibu
kila mwaka inashiriki Ligi ya Mabingwa.
Dili la
Ngassa kwenda Merreikh awali liliingia katika mgogoro, baada ya Azam kumuuza
bila kuishirikisha Simba.
Ikumbukwe, Azam
walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na
kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika
Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi
ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya
hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam
kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara
nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa
kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa
baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji
huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni
30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.