Na Mahmoud Bin Zubeiry |
HASIRA za mashabiki wa
soka Tanzania zi wazi kwa sasa dhidi ya washambuliaji wawili chipukizi wa timu
hiyo, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu ambao wote wanachezea
Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Wachezaji hao
hawakupatikana katika kikosi cha Bara kilichocheza michuano ya Kombe la Mataifa
ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge Novemba hadi Desemba mwaka
huu na hawakuwapo pia kwenye kikosi cha Muungano, Taifa Stars kilichocheza
dhidi ya Zambia Jumamosi iliyopita.
Kwa sasa, wawili hao
wanachukuliwa kama hawana mapenzi kwa timu yao na mashabiki nchini wameanza
kuonyesha hasira za wazi dhidi yao.
Katika mchezo wa Taifa
Stars na Zambia, wapo mashabiki walibeba mabango ya kuwakandia wachezaji hao,
haswa Samatta.
Siku zote, mtu
anayechukiwa sana ni yule ambaye alipendwa awali- hivyo hata chuki dhidi ya
Samatta zinatokana na kwamba Watanzania walimpenda sana, wakamuunga mkono na
kumtakia kila la heri katika jitihada zake za kusaka mafanikio kisoka.
Watanzania walitarajia
makubwa kutoka kwake- kwamba angeisaidia mno timu ya taifa, angeitangaza nchi
katika dunia ya soka kupitia mafanikio yake binafsi kutokana na kipaji chake.
Lakini sasa hayo
yameingia doa, kutokana na chuki hizo zilizoibuka dhidi yake na mwenzake na
Ulimwengu, kwa kutofika katika kambi za taifa wanapoitwa.
Siku zote mimi naamini,
ni vema Watanzania tukawa na utamaduni wa kuyatazama mambo kwa kina, kuyajadili
kwa mapana marefu, ili kuyapatia majibu sahihi katika lengo ya kuyatatua.
Kwa sababu hiyo, sioni
kama kuna mantiki yoyote kwa sasa kwetu kuanza kujenga chuki dhidi ya Samatta
na Ulimwengu bila kupitia hatua hizo za msingi. Hawa vijana bado wadogo na kwa
hakika taifa bado linawahitaji sana ni vema kuwa nao pamoja, kuliko kutaka
kutengeneza mtafaruku.
Sioni kama suala hilo
limefikia huko tunapotaka kulifikisha, zaidi ya kutaka kuzipa nafasi hasira
kufanya kazi kuliko hekima na busara.
Nataka nikumbushe kitu
kimoja, suala la hawa wachezaji kuja katika kambi za taifa linatokana na ruhusa
ya klabu yao, Mazembe.
Niliwahi kufanya
mahojiano na Makamu wa Rais wa Mazembe, Mohamed Kamwanya kuhusu kuchelewa kwa Ulimwengu
kuingizwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, ambaye alisema kwamba
mshambuliaji huyo alichelewa kwa sababu ya kiwango chake.
Alisema kwamba,
Ulimwengu kila anapopewa ruhusa ya kurejea Tanzania kujiunga na timu za taifa,
kwanza huchelewa kurudi Lubumbashi na pia hurudi akiwa hayuko fiti.
“Hicho ndio
kinamchelewesha, lakini kama siyo hivyo angekuwa anacheza tu kama mwenzake. Na
nyinyi watu wa vyombo vya habari mtusaidie, kwa sababu wachezaji wakija huko
wanafanya anasa, wanarudi huku hawako fiti, sasa inakuwa mbaya,”alisema
Kamwanya.
Kabla ya hili sakata la
juzi, awali Mazembe ilifikia hatua ya kuwazuia wachezaji wote hao, kurejea Tanzania
kujiunga na timu za taifa, kwa sababu hata Samatta inaelezwa anaporejea
nyumbani, akirudi Lubumbashi anakuwa ameshuka kiwango.
Hali hiyo imetafsiriwa
inatokana na wachezaji hao kufanya anasa wanapokuwa Dar es Salaam na chanzo ni
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchelewa kuwapa tiketi wachezaji hao,
wanapomaliza majukumu yao ya kitaifa, hivyo wakati wanasubiri tiketi wanaishia
kujirusha, kula bata kwa kwenda mbele.
Kwa kuwa kipindi chote
hicho wanakuwa hawafanyi mazoezi na wanaichosha miili yao kwa anasa, wanapoelekea
Lubumbashi wanampa kazi kocha Lamine N’Diaye kuanza kuwatengeneza upya.
Alipochoshwa na hali
hiyo, N’Diaye aliweka ngumu, Uli hakurudi nyumbani kuichezea timu ya taifa ya
vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes na kwa kumkosa mpachika
mabao wake huyo tegemeo, sisiti kusema ilichangia kwa kiasi kikubwa kutolewa na
Nigeria katika mbio za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika.
Hilo liliwafanya TFF,
walalamike sana hasa baada ya kumpiga ‘stop’ na Samatta pia kujiunga na kambi
ya timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi
ya Botswana, ambao uliisha kwa sare ya 3-3 mjini Gabarone hadi kutishia
kulifikisha suala hilo Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwani wamekiuka agizo la
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
TFF walisahau kwamba,
Mazembe ilikuwa ina hoja na lalamiko la msingi, ambalo naamini kesi hiyo
ikienda popote, klabu hiyo bingwa Afrika mara nne, itashinda.
Mchezaji ni mali ya
klabu na kanuni zinatoa mwongozo mzuri juu ya ushiriki wao kwenye timu za
taifa, hivyo hata vyama vya soka vina wajibu wa kuzitekeleza kanuni hizo.
Bado wamekuwa hawajali
hata umuhimu wa kuwarejesha mapema wachezaji wa nje baada ya kumaliza majukumu
yao ya kitaifa.
Natambua kuna mambo
mawili hapa katika suala la wachezaji hawa, Samatta kusema anaumwa hawezi
kujiunga na timu na pia kutorejea kujiunga na timu baada ya kuitwa. Nataka sote
tutambue umuhimu wa wachezaji hawa kwanza, kabla ya kuanza kulijadili suala
lao.
Na baada ya hapo, ndipo
twende kwenye hoja ya msingi bila ya jazba, tuanze na kutoonekana kwao kwenye
Challenge na hili la juzi la Zambia.
Samatta amesema
anaumwa, sasa tunapokataa haumwi ina maana tunamchukulia yeye kama roboti au?
Tunataka tu Samatta acheze hata katika mazingira hatarishi, mwisho wa siku tunasahau
historia ya TFF na wachezaji wanapoumia, tangu inaitwa FAT.
Wachezaji wangapi
wamekwishatelekezwa baada ya kuumia na hata wa kizazi cha sasa kiasi cha
wengine kama Stefano Mwasyika kufikia kuapa hatachezea tena timu hiyo?
Lakini pia hatupaswi
kusahau kwamba hawa vijana nao ni binadamu na mchezo wa soka umeundiwa mamlaka
yake inayotambulika kisheria, hivyo kuna namna ya kuwasiliana nao yanapotokea
matatizo kama haya.
Binafsi sikuona umuhimu
wa mchezaji yeyote anayecheza nje kuitwa katika kikosi cha Challenge au
kilichomenyana na Zambia katika wakati huu ambao tunajiandaa na mechi za kufuzu
za CHAN.
Niliona ipo haja ya
kuwa na kikosi ambacho tutakitumia kwenye mechi za kufuzu za CHAN, ambacho
kitaundwa na wachezaji wa nyumbani pekee.
Sijui Kim Poulsen
amekuwa na woga kiasi gani hadi katika mechi kama hizi ambazo anapaswa kuandaa
timu ya kumpigania kwenye mashindano mengine muhimu, anataka kuchanganya
madawa.
Lakini hiyo si hoja
yangu leo, yalikuwa mapitio tu. Hoja yangu leo ni kuhusu Samatta na Ulimwengu,
tusiwahukumu kabla ya kulitazama kwa jina suala lao na kulijadili kwa mapana
marefu.