Oloya |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KIUNGO wa
Uganda, Moses Oloya amesema kwamba yupo tayari kuachana na klabu yake, Saigon
Xuan Thanh ya Vietnam na kujiunga na Yanga SC ya Dar es Salaam, ambao watampa
maslahi mazuri.
Yanga SC
inamfuatilia mchezaji huyo katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati,
CECAFA Tusker Challenge kwa ajili ya kumsajili, akazibe pengo la kiungo wake
Mnyarwanda, Haruna Niyonzima anayetakiwa na El Merreikh ya Sudan.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Uwanja wa Mandela, Namboole baada ya kuiongoza nchi yake,
kuifunga Ethiopia mabao 2-0, Oloya alisema kwamba kama Yanga watafika Kampala na
kuzungumza naye, wakiafikiana atahamishia maisha yake Dar es Salaam.
“Nimebakiza
mkataba wa mwaka mmoja katika klabu yangu, lakini tukikubaliana naweza kuondoka
Vietnam bila masharti magumu, Yanga waje tu tuzungumze,”alisema.
Kiongozi mmoja
wa Yanga, jana aliiambia BIN ZUBEIRY kwa simu jana kutoka Dar
es Salaam kwamba, wanafuatilia maendeleo ya Oloya katika michuano hiyo na iwapo
ataendelea kufanya vizuri watakuwa tayari kumsajili.
“Unajua
Haruna ana asilimia kubwa ya kuondoka, sasa lazima tupate kiungo mbadala mzuri
kama yeye na mzoefu, tumefuatilia kwa haraka haraka tumemuona huyu Oloya, ngoja
tuendelee kumuangalia,”alisema kiongozi huyo.
Oloya alizaliwa
Oktoba 22, mwaka 1992 na kabla ya kujiunga na Saigon Xuan Thanh mwaka 2010, aliichezea
KCC ya nyumbani kwao tangu mwaka 2009. Kiungo huyo alianza kuichezea Uganda
mwaka jana na sasa amekuwa tegemeo la timu hiyo.