Rais wa TFF, Leodeagr Tenga |
Na Prince Akbar
RAIS wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hakuna hila yoyote
katika nia ya kutaka marekebisho matatu kwenye katiba kabla ya uchaguzi na
kuwataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mabadiliko hayo kwa maslahi ya
maendeleo ya mchezo huo.
Tenga
alisema hayo leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam,
kufafanua juu ya waraka wa kuomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF
kuridhia mapendekezo matatu ya mabadiliko ya katiba yanayohusu uingizaji wa
kipengele cha utoaji leseni kwa klabu (Club Licensing); kuundwa kwa Kamati ya
Rufaa ya Uchaguzi wa TFF na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF.
Hatua ya
kutuma waraka wa kuomba ridhaa ya mabadiliko hayo imetafsiriwa tofauti na
baadhi ya wadau, wengine wakisema ni mbinu za uongozi wa sasa kutaka uendelee
kukaa madarakani wakati wengine wakitaka ufafanuzi wa vipengele hivyo.
“Hakuna hila
hata kidogo. Yote ni mambo ya maendeleo na nia yetu ni kufanikisha ili mambo
yaendelee,” alisema Rais Tenga kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
“Tusifikie
sehemu tukaanza kulaumu kwa nini mtu ametaka maelezo. Lakini sikutarajia kuwa
mtu wa mpira akiambiwa hili ni agizo la FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa),
atasita; akiambiwa hili ni agizo la CAF (Shirikisho la Soka Afrika), atasita,
au akaambiwa huu ni uamuzi wenu wenyewe, akasita.”
Tenga
alisema nia ya Kamati ya Utendaji ya TFF ilikuwa ni kuitisha Mkutano Mkuu kwa
ajili ya mabadiliko hayo ya katiba, lakini akasema
baada ya
kutafakari kwa kina na kuangaliwa uwezo wa Shirikisho, Kamati iliona haiwezi
kuitisha mikutano miwili kwa sasa kwa kuwa TFF haina fedha.
“Tumetoa
maelezo kuwa tunafahamu kuwa katika mazingira ya kawaida tungeitisha mkutano
mkuu; tuje tuzungumze na baadaye siku ya pili watu waondoke halafu tuwaite tena
kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi,” alisema Tenga ambaye alibainisha kuwa
gharama za chini za mkutano mkuu wa TFF ni kati ya sh. milioni 90 na sh.
milioni 110.
“Lakini
tumeeleza bayana kuwa uwezo huo hatuna, tungelikuwa nao wala tusingefika mahali
hapa; vijana wetu wanahangaika hadi tunatafuta watu watusaidie. Kwa hiyo
tukasema kuna dhambi gani kuwa wakweli. Katiba inasema mkitaka kufanya
mabadiliko ya katiba, itisheni mkutano mkuu. Unaita Mkutano Mkuu kwa sababu
gani, ili mlete wajumbe wa mkutano mkuu ambao ndio watakaopitisha mabadiliko
hayo na ndio maana tumeona dhana hiyo ya kutuma waraka.”
Kuhusu
mabadiliko hayo, Tenga alifafanua kuwa maagizo kuhusu utoaji leseni kwa klabu
(Club Licensing) na kuundwa kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF yalitolewa
mwishoni Julai, ikiwa ni baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji cha Julai na
hivyo suala hilo kulazimika kuzungumzwa kwenye kikao cha Septemba.
Alisema:
”Pamoja na kwamba Tanzania ilishaingiza kwenye kanuni za ligi masharti ya
utoaji leseni, CAF imekuja na maagizo kwamba ni lazima itamkwe kwenye katiba
kuwa TFF itatoa leseni kwa klabu kwa mujibu wa maagizo ya CAF na msipofanya
hivyo klabu zenu hazitaruhusiwa kushiriki mashindano ya klabu ya Afrika
mwakani,”
Simba na
Azam FC zitaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika na
Kombe la Shirikisho, hivyo kutopitishwa kwa mabadiliko hayo mapema
kutasababisha wawakilishi wa Tanzania wazuiwe kushiriki michuano hiyo.
Kuhusu
kuundwa kwa Kamati ya Rufani, Tenga alisema baada ya kuomba ufafanuzi wa utata
uliojitokeza katika vyombo vya maamuzi vya TFF, FIFA ilisema ili kuondoa
mgongano wa kimaslahi, ni muhimu ikaundwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF
badala ya mfumo wa sasa ambao Kamati ya Rufani hujigeuza kuwa Kamati ya Rufani
za Uchaguzi inapofikia wakati wa uchaguzi mkuu wa TFF.
“Kwa hiyo
tunachoomba hapa ni ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba iwepo Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi wa TFF ili kama mtu hatatendewa haki na Kamati ya Uchaguzi
ya TFF, basi akate rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi badala ya chombo
kimoja kushughulikia mambo mawili,” alisema Tenga.
Kuhusu
kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, kiongozi huyo alisema suala
hilo lilitokana na uamuzi wa Mkutano Mkuu uliopita kuwa Ligi Kuu na Ligi Daraja
la Kwanza ziendeshwe na chombo huru.
“Baada ya
hapo Kamati ya Utendaji iliziambia klabu kuwa tunaunda Kanuni za Kuendesha
chombo huru cha ligi, tunaomba mapendekezo yenu. Na ndipo walipotuletea
mapendekezo yao kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi atoke kwenye klabu sita za juu
na kwamba kiwango cha chini cha elimu kiwe Cheti cha Elimu ya Kidato cha Nne
kama ilivyo kwenye katiba,” alisema.
“Maana yake
ni kwamba sifa hizo hazikidhi utashi wa kikatiba wa sifa za mgombea wa nafasi
ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF ambazo ni Elimu ya Chuo Kikuu, lakini klabu
zikasema hazina haja na nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais na ndio maana tunaomba
ridhaa sasa ya kuondoa nafasi hiyo.”
“Napenda
kusema jambo hili ni la maendeleo na hakuna hata moja ambalo si la maendeleo.
Tumepata barua kutoka Kagera ikieleza kuwa utaratibu huu haufai, Katibu Mkuu
amepata na atawajibu. Pwani nao wameomba ufafanuzi na tutatoa waraka wa
ufafanuzi kwa wote.
“Watu wana
haki ya kuhoji na sisi ni wajibu wetu kuwaelimisha. Ombi langu ni tushirikiane
ili twende kwenye mkutano mkuu wetu unaokuja ili tuchaguane. Tukichaguana
tutakuwa tumetimiza jambo muhimu kweli kweli.”
Tenga pia
aliwasihi wajuimbe wa Kamati ya Utendaji kuendelea na jitihada za kuelimisha
wajumbe ili waridhie mabadiliko hayo na shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu
ziendelee kama kawaida.