Deo Munishi 'Dida' |
Na Princess Asia
TIMU ya soka
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeingia kambini jana jioni (Desemba 12 mwaka
huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya
mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) huku Kocha Kim Poulsen akimjumuisha
tena katika kikosi hicho kipa Deogratias Munishi ‘Dida’.
Kocha
Poulsen amemjumuisha tena Munishi kwenye kikosi hicho kuziba nafasi ya Mwadini
Ally ambaye atakuwa nje ya nchi na timu yake ya Azam inayokwenda kushiriki
mashindano maalumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wachezaji
wote wengine walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
wamesharipoti kambini hoteli ya Tansoma, na timu imeanza mazoezi leo asubuhi
(Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, na jioni itafanya mazoezi kwenye
uwanja huo huo.
Kuanzia
kesho jioni (Desemba 14 mwaka huu) itafanya mazoezi Uwanja wa Uwanja wa Taifa
wakati mazoezi ya asubuhi yataendelea kuwa Uwanja wa Karume. Wachezaji ambao
bado hawajaripoti kambini ni Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira
wa kulipwa nchini DRC.
Mechi kati
ya Taifa Stars na mabingwa hao wa Afrika itachezwa Desemba 22 mwaka huu kwenye
Uwanja wa Taifa. Kocha wa Chipolopolo, Herve Renard ameshataja kikosi chake cha
wachezaji 24 kwa ajili ya mechi hiyo.