Abbel Dhaira |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA namba
moja wa Uganda, Abbel Dhaira kwa sasa ndiye mlinda mlango, anayelipwa mshahara
mkubwa zaidi Tanzania, kufuatia mkataba aliosaini juzi na klabu yake mpya,
Simba SC ya Dar es Salaam.
Dhaira,
aliyesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola za Kimarekani 40,000,
atakuwa anapokea mshahara wa Sh. Mlioni 2 kwa mwezi, hivyo kuwapiku makipa
waliokuwa wanalipwa zaidi nchini, Juma Kaseja wa Simba na Mghana, Yaw Berko wa
Yanga, wanaolipwa Sh. Milioni 15.
Dhaira
alisaini mkataba juzi katika hoteli ya JB Belmonte, Dar es Salaam mbele ya
Katibu wa Simba, Evodius Mtawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu
hiyo, Zacharia Hans Poppe.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY juzi, baada ya kumsajili kipa huyo, Hans Poppe alisema kwamba
huyu ni kipa wa kwanza mwenye umbo kubwa tangu, kumalizika kwa zama za Mwameja
Mohamed katika klabu hiyo.
“Naamini
tumepata mtu sahihi na katika wakati mwafaka, hakuna asiyejua umahiri wa Dhaira
langoni, sasa tunasubiri kuvuna matunda ya kumsajili,”alisema Hans Poppe,
Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), ambaye aliondoka jana
nchini kwenda Uingereza kwa mapumziko ya Krisimasi na mwaka mpya.
Hans Poppe aliyepigana
vita dhidi ya Uganda, alisema kwamba Dhaira ni kipa ambaye amependekezwa na
kipa wao wa kwanza hivi sasa, Juma Kaseja hivyo anaamini wawili hao wataishi
vizuri na kushirikiana.
Kwa upande
wake, Dhaira ambaye alirejea jana kwao Uganda kwenda kuchukua vifaa vyake vya
kazi kwa ajili ya kuja kuanza kumtumikia mwajiri wake mpya, alisema kwamba
amefurahi kusaini Simba SC na atafanya vizuri ili kuwafurahisha mashabiki wa
klabu hiyo.
“Simba ni
klabu kubwa Afrika na inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika, kuna wachezaji rafiki
zangu na ndugu zangu, Mussa Mudde na Emmanuel Okwi, lakini Afrika Mashariki ni
moja, wachezaji wote wa Simba ni ndugu zangu, nitajisikia nipo nyumbani kabisa”alisema
Dhaira, anayetua Simba akitokea I.B.V FC ya Iceland.
Dhaira
aliyeibukia Express ya Uganda mwaka 2006, mwaka 2008 alihamia U.R.A. pia ya
Uganda, ambayo aliichezea hadi mwaka 2010 alipohamia Ulaya.
Kwa kumpata
Dhaira, Simba SC imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza,
Juma Kaseja ambaye amekuwa akisoteshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo
inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha
uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako
ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.