Dhaira |
Na Mahmoud Zubeiry
KIPA Abbel
Dhaira amesema kwamba hawezi kujihesabu kama tayari yeye ni kipa wa Simba hadi
hapo watakaposaini mkataba, kwani kwa sasa wamezungumza na kufikia makubaliano,
ila ikitokea timu nyingine ya kumaliza naye haraka, hatasita kufanya hivyo.
“Simba
wamezungumza na mimi ndio, lakini hatujamalizana, wao wakituma mtu kuja huku
tukasaini, hapo ndio nitakuwa nimejifunga, ila kwa sasa kama ipo timu nyingine
hata huko Tanzania inanitaka, milango bado iko wazi,”alisema Dhaira.
Dhaira
alisema kimsingi yeye yuko tayari kujiunga na Simba kwa kuwa ni klabu kubwa
Afrika na inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na angependa kuungana na Mganda
mwenzake, Emmanuel Okwi huko.
Inaonekana
Dhaira kama hawaamini Simba SC na kwa sababu hiyo ana wasiwasi anaweza kukataa
ofa nyingine na Wekundu hao wa Msimbazi wakashindwa kumalizana naye.
Tayari Simba
SC imefikia makubaliano na kipa huyo namba moja wa Uganda, aliyemaliza mkataba wake
na klabu ya I.B.V FC ya Iceland na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili
kwa dau ambalo halijafahamika.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Dhaira alisema kwamba amefikia makubaliano na Simba
kusaini mkataba wa miaka miwili kuja kuanza maisha mapya Dear es Salaam.
“Kila kitu
safi, nasubiri wanitumie tiketi niende Dar es Salaam kusaini,”alisema Dhaira.
Alipoulizwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kuhusu
mchezaji huyo, alisema; “Kweli, atakuja kusaini wakati wowote hapa,”alisema
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Dhaira
ambaye aliibukia Express ya hapa mwaka 2006 kabla ya 2008 kuhamia U.R.A. pia ya
hapa, ambayo aliichezea hadi 2010 alipohamia Ulaya atatua Dar es Salaam
Jumatatu kumaliza kila kitu Simba.
Kwa kumpata
Dhaira, Simba SC imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza,
Juma Kaseja ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo
inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha
uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi
za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja
alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha
mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili
katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu
hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema
hataki tena kuchezea Simba.
Lakini
pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako
ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.