Kijukwaa cha VIP cha Lugogo, nyuma yake kuna kanyumba ka kukabadilishia nguo wachezaji |
KUFUATIA mvua mfululizo zilizonyesha mjini Kampala, Uganda
wiki hii, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) liliamua
kuzihamishia baadhi ya mechi za michuano ya CECAFA Tusker Challenge kutoka
Uwanja wa Mandela, Namboole, hadi Lugogo.
Lengo la kufanya hivyo ni kuupumzisha Uwanja wa Namboole,
ambao ulikwishakuwa na hali mbaya kutokana na mvua hizo.
Na Mahmoud Bin Zubeiry |
Wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kutangaza mabadiliko
hayo, Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye alijikuta kwenye wakati mgumu kwa
maswali ya wana Habari, waliohoji kwa nini mashindano yapelekwe kwenye viwanja
vya uchochoroni.
Waandishi wa kigeni waliishambulia Uganda kwamba haikuwa na
sifa za kupewa uenyeji wa mashindano hayo, kwa sababu baada ya Namboole
kuharibika kwa mvua, Uwanja mwingine, Nakivubo nao upo katika ukarabati.
Wakati akishambuliwa kwa maswali, Ofisa Habari wa Shirikisho
la Soka Uganda (FUFA), Rodgers Mulindwa alisema kwamba wanakabiliwa na tatizo
ambalo ni kutokuwa na viwanja.
Mulindwa alisema kwamba, FUFA haina Uwanja, viwanja vyote ni
mali ya serikali, hivyo hawana mamlaka navyo.
Hiyo ni hali ambayo inalikabili hata Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), viwanja vyote nchini ni mali ya serikali na CCM, chama tawala.
Tuachane na hayo- kikubwa kilichonivutia ni baada ya kuhamishiwa kwa mechi
Askari wakilinda moja ya maageti ya Uwanja huo |
Mashabiki wanakula bia zao za kopo huku mechi ikiendelea |
hizo
kwenye viwanja vidogo vidogo kama huo wa Lugogo, uliopo mjini tu.
Ni Uwanja ambao kwa mechi ambazo hazina mashabiki wengi,
unafaa mno. Wakati nikishuhudia mchezo kati ya Tanzania Bara na Somalia na
baadaye Rwanda na Eritrea kwenye Uwanja huo jana, pia nilikuwa nikizungusha
shingo yangu kuutazama vizuri.
Nilirudisha hisia zangu Dar es Salaam na kuvitafakari viwanja
kama TCC pale Chang’ombe, Leaders Club, Kinesi, Tandika Mabatini, Bandari au
pale palipokuwa panaitwa Kidongo Chekundu, Mnazi Mmoja.
Uwanja wa Lugogo, umezungushiwa seng’enge ya uzio wa kutenganisha
mashabiki na eneo la kuchezea mpira. Una kijukwaa fulani kidogo tu upande mmoja.
Una jengo dogo la vyoo na vyumba vya kubadilishia nguo kwa timu.
Kali kuliko yote, una nyasi nzuri zilizopendeza zinazofaa mno
kuchezea kandanda. Niliupenda. Nilipoutazama mara mbili mbili ukubwa wake,
sikuona tofauti yeyote na viwanja vya Dar es Salaam nilivyovitaja hapo juu.
Angalia mashabiki nyuma ya goli kabisa |
Viti vya kukalia wachezaji wa akiba |
Dar es Salaam kuna kilio kikubwa cha makato ya mapato ya
milangoni kwa mechi zinazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, ambao ni mali ya
serikali na kwa sababu hiyo, baadhi ya timu za mjini zinalazimika kwenda
kuchezea mechi zake nje kabisa ya mji kwa kuwa hazina uwezo wa kufidia gharama
za Uwanja wa Taifa.
Na watu wenye kupenda soka, wanashindwa kuzifuata timu hizo
nje ya mji, kwa sababu ni mbali wanahofia muda na gharama.
Najaribu kutafakari, kama Ilala itakuwa na viwanja vidogo
japo vitatu, Kidongo Chekundu, Muhimbili na Karume, ambavyo vitatengenezwa
vizuri na kuoteshewa nyasi mfano wa Lugogo, tutakuwa tumepunguza tatizo kwa
kiasi gani?
Temeke nako, pamoja na kuwapo Uwanja wa Taifa, lakini pia
TCC, Bandari na Tandika Mabatini navyo vikafanyiwa ukarabati, je hali itakuwa
nzuri kwa kiasi gani?
Tazama mashabiki wanavyokaa kwenye Uwanja huo |
Jukwaa la upande wa pili la Lugogo |
Kinondoni nako, viwanja vya kule mfano ule wa Chuo cha Ustawi
wa Jamii, TPDC, Posta, Kinesi, Ufi au hata mwingine wowote, vikifanyiwa
ukarabati wa aina hiyo, mambo yatakuwaje?
Ninachokiona hapa, huu mzigo wa TFF bali serikali ya Jiji la
Dar es Salaam kubeba jukumu la kuvikarabati viwanja hivyo. Nawashauri, viongozi
wa Jiji la Dar es Salaam, wasafiri waje Kampala, siyo tu kuitazama Lugogo ili
wajifunze nao namna ya kuboresha viwanja vya jiji hilo, bali na mambo mengine
pia, ikiwemo muundo wa Jiji na usafi kwa ujumla. Kampala ya leo inavutia bwana
pamoja na foleni ndefu zisizokatika.
Narudisha kumbukumbu zangu nyuma, miaka ya 1990 wakati Uwanja
wa Karume ulipokuwa unatumika kwa mechi za timu ndogo za katikati ya Jiji,
mfano Pentagon, Boom, Ashanti, Kumbukumbu na Cosmo, mashabiki walikuwa
wanafurika uwanjani kwa sababu zinacheza maeneo ya karibu na maskani zao.
Lakini leo Ashanti ikirudi Ligi Kuu, itacheza mechi nne tu
Uwanja wa Taifa na dhidi ya Simba na Yanga, nyingine zote sijui itapelekwa
Chamazi, wangapi watakwenda? Hata African Lyon leo ingekuwa inachezea mechi
zake Uwanja wa TCC, wangekuwa wanapata watu uwanjani.
Pande nyingine mbili mashabiki wanasimama tu Lugogo |
Ni Uwanja simpo sana |
Uongozi wa Jiji la Dar es Salaam unapaswa kujua viwanja ni
uwekezaji mzuri kwa maslahi ya taifa, tena makubwa sana. Leo ni timu kubwa za Dar es Salaam zinahaha
sehemu za kufanyia mazoezi, lakini kama Jiji lingekuwa lina viwanja vya
kutosha, lingekuwa linaingiza kiasi gani cha fedha?
Usisahau pia kuwepo kwa viwanja vingi vyenye hadhi, kutavutia
vijana wengi kucheza soka na hivyo kutengeneza vipaji vingi zaidi. Je, Jiji
wanaangalia yote hayo?
Tena siku hizi viwanja vinazungukwa na vyumba vya biashara
kama maduka na sehemu za vinywaji labda, zote hizo ni fedha ambazo Jiji
linazikosa kwa sasa kwa kukosa ubunifu. Wenzetu wanasoma sana ili kuongeza
ujuzi na waweze kufanya kazi kwa ufanisi, lakini Watanzania tulio wengi
tunasoma ili kutengeneza hadhi tu tuweze kuwa mabosi tunaolipwa mishahara
makubwa, na si kufanya kazi nzuri. Tatizo hilo na lazima tubadilike.
Mh Juma Nkamia katikati akiwa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura wakitazama mechi jana Lugogo |
Rwanda na Eritrea Lugogo jana |
Juzi tu hapa Kampala ulikuwa mji usiovutia hata kidogo,
lakini leo imebadilika mno na hapa wanaostahili pongezi ni wenye mji wao, vipi
sisi na Dar es Salaam yetu? Hapana, Dar es Salaam inaweza kuwa kabisa sawa na
Kampala, iwapo uongozi wa Jiji utaamua kufanya kazi ya kuboresha mambo
mbalimbali, likiwemo suala la viwanja. Jumapili njema.