Na Prince Akbar
TIMU ya Coastal
Union ya Tanga imeendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kuwania Kombe la
Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi
Kuu ya Vodacom baada ya jana (Desemba 12 mwaka huu) kuifunga Toto Africans
mabao 3-1.
Mabao ya
Coastal katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Chamazi yalifungwa
na Mohamed Miraji dakika ya 44, Abdul Banda (dk. ya 62) na Ramadhan Shame (dk.
ya 83). Toto Africans ndiyo iliyoanza kupata bao dakika ya 30 lililofungwa na
Severin Constantine.
Coastal
Union ilishinda mechi yake ya kwanza mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika
michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji
Uhai.
Nayo Simba
iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon katika mechi ya kundi B
iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 12 mwaka huu) Uwanja wa Karume. Miraji Athuman
na Ramadhan Mzee ndiyo walioifungia Simba dakika ya 15 na 47 wakati la African
Lyon lilifungwa dakika ya 57 na Mbela Kashakala.
Polisi
Morogoro iliifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume wakati katika Uwanja wa
Azam, JKT Ruvu iliifunga Tanzania Prisons bao 1-0 lililofungwa dakika ya 16 na
Jacob Mambia. Yanga na Ruvu Shooting zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Chamazi.
Katika mechi
iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Oljoro JKT
imeizamisha Kagera Sugar mabao 3-0. Mabao hayo yamefungwa na Hamis Saleh dakika
ya 49 huku Shamir Mohamed akipachika mawili dakika ya 52 na 55.
Michuano
hiyo itaendelea kesho (Desemba 14 mwaka huu) kwa michezo kati ya Mtibwa Sugar
vs Toto Africans (asubuhi- Karume), Coastal Union vs JKT Ruvu (mchana- Karume),
Oljoro JKT vs Yanga (asubuhi- Chamazi), Ruvu Shooting vs Kagera Sugar (mchana-
Chamazi), Mgambo Shooting vs Simba (asubuhi- Chamazi) na African Lyon vs Azam
(jioni- Chamazi).