Cannavaro |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
NAHODHA wa
Zanzibar, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikuwapo jana Uwanja wa Mandela, Namboole
akiishuhudia Kenya ikiichapa Malawi 2-0 na kutinga Fainali, lakini amesema Harambee
Stars ‘weupe tu kwao’.
Akizungumza
jana baada ya mechi hiyo, Cannavaro alisema kwamba kulingana na kiwango
kiliochoonyeshwa na Kenya katika mechi hiyo dhidi ya Malawi, wanaamini
watawafunga.
“Yaani jamaa
weupe sana, hata bao walilopata la kibahati bahati sana, mimi nakuambia sisi
hawa tunawafunga, timu yetu nzuri sana,”alisema beki huyo wa kati wa Yanga SC
ya Dar es Salaam.
Nahodha huyo
wa Yanga SC, alisema kwamba baada ya kuitoa Burundi juzi sasa anaamini Kombe la
Challenge litakwenda Zanzibar, kwani haoni timu nyingine ya kuwasumbua wao
katika mashindano haya.
Zanzibar juzi
ilikata tiketi ya kutinga Nusu Fainali baada ya kuichapa Burundi kwa penalti 6-5
kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 na sasa itacheza na mshindi
kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
Shujaa wa
Zanzibar juzi alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya
kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha wa
timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa
Burundi walipoteza penalti zao juzi.
Ndikumana
alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya
lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo,
Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
Upande wa
Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya
Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu,
kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa
Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na
Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.