Cannavaro |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
NAHODHA wa
Zanzibar, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ amesema kwamba hawawahofii hata kidogo
Burundi japokuwa hawajafungwa hata mechi moja kwa sasa katika mashindano ya
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, yanayoendelea
mjini hapa.
Zanzibar
Heroes, ambayo haina wadhamini, itapambana na Burundi kesho katika Robo Fainali
kwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa, mchezo ambao utatanguliwa Robo Fainali
nyingine kati ya Tanzania Bara na Rwanda.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana mjini hapa, beki huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam,
alisema kwamba anakubali Burundi ni timu nzuri, lakini watapigana kiume
kuhakikisha wanashinda na kuingia Fainali.
“Sisi
tumekuja hapa kuchukua Kombe, kwa hivyo hatuhofii timu yoyote, ndiyo Burundi
wazuri, wameifunga Bara, lakini sisi ni Zanzibar, na tutapambana kiume
tuwatoe,”alisema Cannavaro.
Akiuzungumzia
mchezo wa jana ambao walifungwa 2-0 na Malawi, Cannavaro alisema kwamba
hawakutaka kutumia nguvu nyingi kwa sababu walikuwa wana uhakika wamekwishafuzu.
“Sisi baada
ya kuona kwamba tunaongoza Kundi kabla ya mechi za mwisho na kupiga hesabu zetu
vizuri baada ya matokeo ya mwisho, tutafuzu tu, tukaamua tusitumie nguvu
nyingi, ili zije kutusaidia katika Robo Fainali,”alisema Cannavaro.