Cannavaro |
Na Princess Asia
NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amerejeshwa kwenye
kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars baada ya kung’ara
katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mjini
Kampala, Uganda.
Katika michuano hiyo, Cannavaro ambaye pia Nahodha wa Zanzibar,
aliiongoza timu hiyo kushika nafasi ya tatu katika michuano iliyoanza Novemba
24 na kufikia tamati Desemba 8, mwaka huu. Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mdenmark,
Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 24, ndani yake akiwatema chipukizi aliokuwa
akiwakomaza kwenye timu hiyo, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Edward Christopher,
wote wa SImba SC.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo ofisi za Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Poulsen alisema kikosi hicho kitaingia kambini keshokutwa
kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa
Afrika, Zambia, Chipolopolo itakayochezwa Desemba 22, mwaka huu Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Mbali na Cannavaro na Aishi Mangula, nyota wengine wapya
walioitwa katika kikosi hicho ni pamoja na Hamisi Mcha ‘Vialli’ na Samir Hajji Nuhu
wote wa Azam FC.
Wengine walioitwa ni makipa; Juma Kaseja (Simba) na Mwadini
Ally (Azam FC), mabeki; Amir Maftah (Simba), Shomari Kapombe (Simba), Erasto
Nyoni (Azam), Nasoro Masoud ‘Chollo’ (Simba) na Aggrey Morris wa Azam FC.
Viungo ni Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho Ngassa (Simba),
Frank Domayo (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athumani Idd ‘Chuji’ (Yanga), Shaaban
Nditi (Mtibwa Sugar), wakati washambuliaji ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu (TP
Mazembe, DRC), John Bocco (Azam), Simon Msuva (Yanga).