Simba SC |
Na Prince Akbar
SHIRIKISHO
la Soka Afrika (CAF) litatuma ofisa wake nchini mwezi ujao kwa ajili ya kufanya
ukaguzi kwenye klabu za Ligi Kuu ya Tanzania kabla ya kutoa leseni kwa zile
ambazo zitakuwa zimekidhi vigezo vilivyowekwa. Ili klabu ishiriki mashindano ya
CAF ni lazima iwe na leseni hiyo.
Kwa mujibu
wa CAF, ofisa huyo atakuwa nchini kuanzia Januari 7 mwakani ambapo atafanya
ukaguzi huo hadi Januari 14 mwakani. Mbali ya ukaguzi katika klabu, pia ofisa
huyo atakagua viwanja vitakavyotumika katika mashindano yake na hoteli ambazo
timu kutoka nje zitakuwa zinafikia kabla ya mechi.
Baadhi ya
masharti kabla ya klabu kupewa leseni ya CAF ni pamoja na kuwa na ofisi (physical
address), uwanja wake wa mazoezi, programu ya maendeleo kwa vijana,
sekretarieti ya kuajiriwa, hesabu za fedha zilizokaguliwa (audited accounts) na
benchi la ufundi linaloundwa na watu wenye sifa zinazostahili.