Diwani wa Kata ya Boko, Sharrif Majisafi (kushoto) akimkabidhi Kombe Nahodha wa Basihaya, Akilimali Bashir jioni hii kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Boko |
Na Mahmoud Zubeiry
TIMU ya
Basihaya Stars leo imeibuka bingwa wa michuano ya Kombe la Diwani Sharrif
Majisafi baada ya kuifunga Bunju Stars mabao 2-0 katika mchezo wa fainali
uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Boko, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam.
Kwa ushindi
huo, timu hiyo imezawadiwa pikipiki yenye thamani ya Sh. Milioni 1.9, seti ya jezi
yenye thmani ya Sh. 300,000, Kombe na mpira, wakati washindi wa pili walipata
seti ya jezi ya thamani ya Sh. 200,000, Kombe na mpira na mshindi wa tatu, Boko
Kati alipata seti ya jezi ya Sh, 200,000, Kombe na mpira.
Katika mchezo
huo, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila nyavu kutikisika na
kipindi cha pili ndipo Basihaya waliokuwa wakicheza ‘barazani kwao’ walipochangamkia
nyavu.
Shujaa wa
timu hiyo inayoundwa na vijana wengi chini ya umri wa miaka 20, alikuwa Shaaban
Abesh aliyefunga mabao yote hayo katika dakika za 64 na 77.
Bunju ilizinduka
baada ya kufungwa mabao hayo ya ‘chap chap’ na kushambulia kwa nguvu langoni
mwa wapinzani wao, lakini bahati haikuwa yao.
Mgeni rasmi
na mwandaaji wa mashindano, Diwani Majisafi alikabidhi Kombe kwa bingwa na
fedha, wakati waalikwa wengine, Mama Janet Rite, Diwani wa Kata ya Kunduchi
alikabidhi kwa washindi wa tatu, Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Kinondoni,
Jumanne Mrimi alikabidhi zawadi za washindi wa pili.
Dullah Carlos
aliyeibuka mfungaji bora kwa mabao yake sita, alizawadiwa mpira.
Mechi hiyo
ilivutia mamia ya wakazi wa Boko na meneo jirani na kwa ujumla uwanja wa
ulipendeza kutokana na idadi kubwa ya akina mama, baba na watoto waliojitokeza.
Vimbwanga vya
aina mbalimbali vya mashabiki vilikuwa sehemu ya burudani kwenye Uwanja huo,
wengine walilewa chakari hadi kumwaga bia mithili ya shampeni wakati
wakishangilia na kali zaidi ni njemba iliyoibuka na ngedere. Upadne wa vyoo vya
shule, ilikuwa ni mioshi na harufu ya bangi tu ya masela waliokuwa wakifuatilia
mechi kwa mbaaali. Ilikuwa burudani.
Kipute |
Zawadi ya pikipiki inatolewa |
Cheki watoto |
Pati la ubingwa |
Mabingwa |
Kuumia huku halafu hakuna ushindi, mchezaji wa Bunju |
Mchizi na ngedere wake |
Mama Zero anamwaga bia kwa furaha |
Mama Zero na patna wake wanamwaga bia kwa raha zao |