Na Abubakar Mapwisa,
Kinshasa
AZAM FC ya
Dar es Salaam, jana imetwaa ubingwa wa Kombe la Hisani, linaloandaliwa na
FECOFA, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya
kuwafunga wenyeji Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs mjini hapa.
Azam walikuwa
wa kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha dakika ya
75.
Katika mikwaju
ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili ya Dragons, wakati Gaudence
Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji Nuhu walifunga penalti za Azam.
Hata hivyo,
Azam jana hawakukabidhiwa Kombe uwanjani hapo baada ya waandaji kusema wanakwenda
kulipamba kwanza, hivyo sherehe za makabidhiano ya Kombe zinaweza kufanyika leo.
Azam jana ilicheza
bila kocha wake Mkuu, Muingereza Stewart Hall ambaye aliondoka juzi usiku mjini
hapa kwenda kwao Uingereza kwa ajili ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY kabla ya kuondoka mjini hapa, Stewart alisema kwamba anamuachia
timu hiyo msaidizi wake, Kali Ongala na anaamini atafanya kazi.
Stewart
alisema Kali ni mtu ambaye siku zote amekuwa akimuandaa kuwa kocha wa baadaye
wa Azam na hii si mara ya kwanza kumuachia timu, kwani aliwahi kufanya hivyo
mara kadhaa ikiwemo kwenye Kombe la Urafiki, ambalo aliiongoza timu kufika
Fainali.
“Siku moja
nitaondoka Azam na kumuacha Kali awe kocha Mkuu, siku zote namtayarisha,
namjengea kujiamini, naamini atakuwa kocha bora sana wa Azam, sina wasiwasi naye,
namuachia timu na anaweza kurudisha Kombe Dar es Salaam,”alisema Stewart ambaye
atarejea mwakani.
Azam iliingia
fainali, baada ya juzi kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya
hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs. Azam inatarajiwa
kuondoka hapa kesho mchana kurejea Dar es Salaam.
Katika
mchezo wa jana, kikosi cha Azam kinatarajiwa kuwa; Mwadini Ally, Himid Mao,
Samih Hajji Nuhu, Joackins Atudo, David Mwantika, Jabir Aziz, Kipre Balou, Seif
Abdallah/Uhuru Suleiman, Kipre Tchetche/Zahor Pazi, Humphrey Mieno na Gaudence
Mwaikimba.