Benchi la Ufundi la Azam, kutoka kulia Daktari Mjerumani, Paulo Gomez, Kocha wa Makipa Mzalendo Iddi Abubakar, Kocha Msaidizi Muingereza Kali Ongala na Kocha Mkuu, Mungereza pia, Stewart Hall |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
SHIRIKISHO
la Soka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), limeigeuzia kibao Azam FC na sasa
linaitaka icheze mechi moja zaidi ili kuwania Nusu Fainali ya michuano ya Kombe
la Hisani inayoendelea hapa.
Hatua hiyo,
inafuatia timu ya Diables Noirs ya Kongo Brazzaville kutofika kwenye mashindano
haya na kufanya Kundi A libaki na timu tatu sawa na B.
Kwa mantiki
hiyo, Azam kesho itashuka tena dimbani kumenyana na FC MK ya hapa mchezo ambao
itatakiwa lazima kushinda ili kurudi Nusu Fainali.
Kabla ya
mabadiliko haya, Azam jana ilifanikiwa kuingia Nusu Fainali baada ya kuilaza Real
de Kinshasa kwenye Uwanja wa Martyrs.
Shukrani
kwao, washambuliaji Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah waliofunga mabao hayo,
moja kila kipindi.
Ikiongezewa
nguvu na nyota wake watatu, Kipre Tchetche, Kipre Balou raia wa Ivory Coast na
Mkenya, Joackins Atudo waliochelewa mechi mbili za awali, Azam leo ilitawala
mchezo na kama si rafu za wapinzani wao, ingevuna ushindi mtamu.
Hadi
mapumziko, tayari Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na
Mwaikimba dakika ya 21, ambaye aliunganisha pasi nzuri ya Kipre kutoka wingi ya
kushoto.
Hilo
linakuwa bao la pili kwa Mwaikimba, mshambuliaji wa zamani wa Kahama United,
Ashanti United, Yanga, Prisons na Kagera Sugar katika mechi tatu za mashindano
haya alizocheza, awali alifunga katika sare ya 1-1 na Dragons.
Kipre
Tchetche alilazimika kutoka nje ya Uwanja dakika ya 43 kutokana na rafu za
wachezaji wa Real, nafasi yake ikichukuliwa na Samih Hajji Nuhu.
Real
walikuwa wakipiga kiatu haswa na kiungo Waziri Salum aliungana na Kipre
Tchetche kuuacha Uwanja kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo, ingawa nafasi yake
ilichukuliwa na Uhuru Suleiman dakika ya kwanza ya kipindi cha pili.
Awali ya
hapo, refa Madila Achille alimtoa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43 beki
Muipalayi Igongo kwa kumchezea rafu mbaya Gaudence Mwaikimba, ambayo chupuchupu
naye imtoe nje, kiasi cha kulazimika
kumalizia mechi akichechemea.
Kipindi cha
pili, Azam waliendelea kuwafundisha soka Real na katika dakika ya 73, kazi
nzuri ya Mwaikimba ilisaidia kupatikana bao la pili. Mpira mrefu uliopigwa na
kipa Mwadini Ally, Mwaikimba aliumiliki vema, akatoa pasi pembeni kushoto kwa
Hajji Nuhu ambaye aliingia ndani kidogo na kukata krosi maridadi iliyounganishwa
kimiani na Seif.
Humphrey
Mieno alikuwa mwathirika mwingine wa rafu za Real, baada ya kulazimika kutoka
nje dakika ya 77, akimpisha Abdi Kassim ‘Babbi’.
Azam
walionekana kuridhika baada ya kuwa wanaongoza mabao 2-0 na wakafanya uzembe
uliowapa bao la kufutia machozi Real, lililofungwa na Bisole Panzu dakika ya
78.
Baada ya
mechi hiyo, kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall aliwapongeza vijana wake,
lakini akasema anakabiliwa na wakati mgumu katika hatua inayofuata kutokana na
wachezaji wake wanne kuumia leo.
Kocha wa
Real, Sandra Makombele aliwasifu Azam ni timu nzuri na akasema anakubali matokeo,
ingawa aliwapiga kijembe. “Wachezaji wangu wana mazoezi mengi, Azam hawana
mazeozi, wakiguswa kidogo wanaumia, hakukuwa na rafu, ule ni mchezo wa nguvu
kama Ulaya, kocha wao inabidi awape mazoezi mengi wawe wagumu,”alisema
mwanamama huyo.
Katika mechi
zake mbili za awali za Kundi B, Azam ilitoka 1-1 na Dragons na ikafungwa 2-0 na
Shark FC.
Azam ilicheza
mechi zote mbili bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na
Msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari
Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory
Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
Watano hao,
waliwasili mjini Kinshasa juzi na beki Joackins Atudo naye aliwasili jana na
wote walishiriiki mchezo wa jana kikamilifu.
Nusu Fainali
zitachezwa Desemba 25 wakati Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka
mshindi wa tatu.