Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Azam
FC imeliandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana ikiwaomba wamruhusu
mshambuliaji Mrisho Ngasa kwenda Sudan kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya
katika harakati zake za kujiunga na El Merreikh ya nchini humo.
Taarifa ya
Azam FC iliyotumwa BIN ZUBEIRY imesema kwamba, katika barua waliyowapelekea TFF,
nakala wamewapelekea pia na Simba SC, ambako mchezaji huyo alikuwa anacheza kwa
mkopo.
“Msukumo
uliotufanya tuandike barua hii ni kwa kutambua kuwa hii ni nafasi muhimu kwa Ngassa
na taifa, kwani anakwenda kucheza kwenye timu yenye uwezo na miundombinu
mikubwa barani Afrika, na inayoshiriki ligi ya mabingwa Afrika karibu kila
msimu, kitu ambacho kitamuongezea Ngassa kiwango na kuwa na msaada kwa tafa,”ilisema
taarifa ya Azam.
Aidha, Azam
wamesema pia wanapenda kuweka wazi thamani ya usajili na mshahara ambao Ngassa.
Wamesema Ngassa atakuwa anapewa na El Merreikh mshahara wa dola za Kimarekani 4,000,
kiasi cha Sh. Milioni 6 za Tanzania kwa mwezi, ambazo kwa miaka miwili ni
takribani Sh. Milioni 144 Milioni.
Wamesema
mchezaji huyo amepewa fedha za kusaini dola za KImarekani 50,000, kiasi cha Sh.
Milioni 80.
“Kwa hiyo
Ngassa ataweka kibindoni zaidi ya Shilingi Milioni 230 kwa miezi 24, hizi ni fedha
nyingi kwa mchezaji wa kitanzania na kwa maendeleo ya mchezaji na familia yake
na yatawapa msukumo vijana wengi wenye kipaji kama Ngassa kufanya bidii kwenye
soka na kuliletea maendeleo taifa,”ilisema taarifa ya Azam.
Azam FC imeomba
TFF imruhusu Ngassa kwenda Sudan akitokea Uganda kwenda kukamilisha vipimo vya
Afya na usajili na Azam FC ipo tayari kukaa na Simba na kuzungumza juu ya
uhamisho huu kwa usimamizi wa TFF.
“Hapa
ieleweke kuwa ingawa Azam FC inajua haki zake kisheria, lakini pia imeamua
kupunguza msimamo wake kukubali mazungumzo kwa kuangalia zaidi athari ambazo
mchezaji anaweza kupata kimaslahi na kimaendeleo ya uchezaji wake na mpira wa
Tanzania kwa ujumla kutokana na mgogoro huu,”iliongeza taarifa hiyo.