Kikosi cha Azam |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
AZAM FC inashuka
dimbani leo kwenye Uwanja wa Martyrs, kumenyana na Real De Kinshasa ya hapa, katika
mchezo maalum wa kutafuta timu ya kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Hisani mjini
hapa, linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka DRC.
Real imeshika
mkia katika Kundi A, wakati Azam pia imeshika mkia katika Kundi B, hivyo zinamenyana
leo kuwania tiketi ya Nusu Fainali.
Azam juzi
ilifungwa mabao 2-0 na Shark FC ya hapa, katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi
B, Kombe la Hisani, kwenye Uwanja wa Martyrs jioni hii.
Mabao ya
washindi, timu inayomilikiwa na mdogo wake rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), Joseph Kabila yalifungwa na Ndibu Kalala dakika ya 23 na Kalala
Kabongo dakika ya 34.
Hata hivyo,
kipigo hicho kilichangiwa kwa kiasi kikubwa na uchezeshaji mbovu wa marefa,
ambao tangu mwanzo walionekana kuwapendelea wenyeji.
Azam juzi walinyimwa
penalti mbili za halali, moja kila kipindi, ya kwanza baada ya shuti la
mshambuliaji Gaudence Mwaikimba kuzuiwa kwa mkono na beki wa Shark na ya pili
kiungo Humphrey Mieno aliangushwa kwenye eneo la hatari, tena ndani ya sita
akiwa amekwishamtoka kipa, lakini zote refa akapeta.
Washika
vibendera nao walizima mashambulizi kadhaa ya Azam kwa kudai wachezaji walikuwa
wameotea.
Mabao yote
Azam walifungwa wakitoka kushambulia na hayakuwa na mushkeli, makosa ambayo
walirekebisha na hawakuyarudia kipindi cha pili. Kipindi cha kwanza, timu
zilishambuliana kwa zamu, lakini kipindi cha pili Azam walitawala zaidi mchezo
na kama si ‘madudu’ ya refa, matokeo yangeweza kubadilika.
Azam ilicheza
mechi zote mbili bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na
Msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari
Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory
Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
Watano hao,
waliwasili mjini DRC jana na leo Azam inatarajiwa kushusha kikosi chake kamili.
Beki Joackins Atudo naye anatarajiwa kuungana na timu leo mjini hapa.
Nusu Fainali
zitachezwa Desemba 25 wakati Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka
mshindi wa tatu. Kundi B, lina timu za
DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa.