Mwaikimba kulia na Hajji Nuhu kushoto; wamo safarini na Azam DRC |
Na Mahmoud Zubeiry
WAWAKILISHI
wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, (CAF), Azam FC
wanaondoka mchana wa leo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kucheza
mashindano ya Kombe la Hisani.
Michuano
hiyo inatarajiwa kuanza leo na itafikia tamati Desemba 23, mwaka huu na Azam FC
itashiriki kwa lengo la kuwapa mazoezi na uzoefu wachezaji wake kabla ya
kuingia kwenye Kombe la Shirikisho mwakani.
Azam pia,
itatumia mashindano hayo kama fursa ya kuwapima wachezaji wake kabla ya kuanza
kwa Kombe la Shirikisho mwakani, ambako wamepangwa kuanza na Al Nasr Juba ya
Sudan Kusini.
Hata hivyo,
katika kikosi cha Azam kitakachoondoka leo, hawamo wachezaji wake wapya wa
kigeni, iliyowasajili beki Mkenya, Joackins Atudo na mshambuliaji Mganda, Brian
Umony.
Mashindano
hayo yatashirikisha timu kubwa za kutoka Kongo kama DC Motema Pembe na A.S.
Vita Club, wakati timu kutoka nje ya Kongo mbali na Azam FC, kuna Tusker FC ya
Kenya, Gombe United ya Nigeria na Diable Noirs ya Kongo Brazzaville.
Kikosi cha
Azam kinachokwenda DRC ni; Mwadini Ally, Jackson Wandwi, Gaudence Mwaikimba,
Himidi Mao, Ibrahim Mwaipopo, Jabir Aziz, Kipre Tchetche, Kipre Balou, Luckson
Kakolaki, Samir Hajji Nuhu, Zahoro Pazi, Seif Abdallah, Malika Ndeule, Omar Mtaki,
Abdi Kassim, Uhuru Suleiman na David Mwantika.
Wachezaji wengine
ambao hawahusiki katika safari hiyo, ni wale waliopo kwenye kikosi cha timu ya
taifa, Khamis Mcha ‘Vialli’, John Bocco ‘Adebayor’ na Salum Abubakar, wakati
wengine ni waliosimamishwa kwa tuhuma za kuhujumu timu, Aggrey Morris, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni ambao wote wapo
timu ya taifa pia na Said Mourad.
Kikosi
hicho kitaongozwa na kocha Mkuu, Muingereza Stewart Hall.