Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Azam
FC imesema kwamba, Simba SC ilikiuka mkataba wao wa kuwauzia kwa mkopo mchezaji
Mrisho Ngassa kwa kitendo cha kumsainisha mkataba nyota huyo na kumpa gari aina
ya Verosa na Sh. Milioni 18.
Taarifa ya
Azam kwa BIN ZUBEIRY, imesema kwamba, wanashangaa Simba kulalamikia Azam
kumuuza El Merreikh ya Sudan bila ya kufikia nao makubaliano, wakati wao
walianza kukiuka mkataba.
“Kwanza
tunapenda umma uelewe kwamba, sisi tuliwashirikisha Simba mapema tu katika
mpango huu, lakini wao wakataka fedha nyingi, ambazo Merreikh hawakuwa tayari
kutoa, na sisi kwa kuzingatia maslahi ya mchezaji na taifa, tukaamua kutumia
haki yetu, akiwa mchezaji wetu kwa kuamua kumuuza,”imesema taarifa ya Azam.
Azam imeliandika
barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juzi ikiwaomba wamruhusu Ngasa kwenda
Sudan kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya katika harakati zake za kujiunga
na El Merreikh ya nchini humo.
Azam FC imesema
kwamba, katika barua waliyowapelekea TFF, nakala wamewapelekea pia na Simba SC,
ambako mchezaji huyo alikuwa anacheza kwa mkopo.
“Msukumo
uliotufanya tuandike barua hii ni kwa kutambua kuwa hii ni nafasi muhimu kwa Ngassa
na taifa, kwani anakwenda kucheza kwenye timu yenye uwezo na miundombinu
mikubwa barani Afrika, na inayoshiriki ligi ya mabingwa Afrika karibu kila
msimu, kitu ambacho kitamuongezea Ngassa kiwango na kuwa na msaada kwa tafa,”ilisema
taarifa ya Azam.
Aidha, Azam
wamesema pia wanapenda kuweka wazi thamani ya usajili na mshahara ambao Ngassa.
Wamesema Ngassa atakuwa anapewa na El Merreikh mshahara wa dola za Kimarekani 4,000,
kiasi cha Sh. Milioni 6 za Tanzania kwa mwezi, ambazo kwa miaka miwili ni
takribani Sh. Milioni 144 Milioni.
Wamesema
mchezaji huyo amepewa fedha za kusaini dola za KImarekani 50,000, kiasi cha Sh.
Milioni 80.
“Kwa hiyo
Ngassa ataweka kibindoni zaidi ya Shilingi Milioni 230 kwa miezi 24, hizi ni fedha
nyingi kwa mchezaji wa kitanzania na kwa maendeleo ya mchezaji na familia yake
na yatawapa msukumo vijana wengi wenye kipaji kama Ngassa kufanya bidii kwenye
soka na kuliletea maendeleo taifa,”ilisema taarifa ya Azam.
Azam FC imeomba
TFF imruhusu Ngassa kwenda Sudan akitokea Uganda kwenda kukamilisha vipimo vya
Afya na usajili na Azam FC ipo tayari kukaa na Simba na kuzungumza juu ya
uhamisho huu kwa usimamizi wa TFF.
“Hapa
ieleweke kuwa ingawa Azam FC inajua haki zake kisheria, lakini pia imeamua
kupunguza msimamo wake kukubali mazungumzo kwa kuangalia zaidi athari ambazo
mchezaji anaweza kupata kimaslahi na kimaendeleo ya uchezaji wake na mpira wa
Tanzania kwa ujumla kutokana na mgogoro huu,”iliongeza taarifa hiyo.
Lakini
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema klabu yake haiko
tayari kufanya mazungumzo na Azam FC juu ya suala hilo.
Kaburu amesema,
klabu yake iliingia mkataba na Azam FC kwa kununua haki zote za huduma za Ngassa
kwa mwaka mmoja, hadi Mei 21 mwakani, ikilipa Sh. Milioni 25 kama ada ya
kumtumia mchezaji huyo kwa mwaka mmoja pamoja na kumlipa mchezaji haki zake
zote stahiki za kimkataba ikiwemo mshahara wake.
Kaburu
amesema Azam bila ya kuzingatia mkataba iliousaini na Simba SC, na matakwa ya
FIFA yanayohusu mkopo, iliamua kutangaza kumuuza Ngassa bila ya kuihusisha Simba
wakati ikijua kuwa ilikuwa na Mkataba na Simba SC ambayo ameishaichezea katika
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara.
“Kitendo cha
Azam FC kuongea na Klabu ya El Merreikh FC na kuweka makubaliano ya mauzo ya
mchezaji na kumtangaza kuwa kimemuuza mchezaji Ngassa bila ya kuihusisha Simba
SC, na baadaye kuiandikia klabu ya Simba kuwa kimeamua kumrudisha mchezaji
Ngassa Azam, wakati ikijua kuwa ina mkataba na Simba SC ni uvunjifu mkubwa wa
taratibu na umeleta athari kubwa kwenye klabu yetu,”alisema Kaburu na kuongeza;
“Tayari
Simba SC ilikwishatuma malalamiko TFF na kupeleka pingamizi lake juu ya sulala
hili kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, ambapo imeamuliwa kuwa suala hili liende
kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji likapatiwe ufumbuzi,”alisema.
Amesema Simba
imekuwa ni klabu yenye kuangalia zaidi maslahi ya wachezaji na haina
kipingamizi kwa kuwaruhusu wachezaji wake kutoka pindi wanapopata timu nje ya
nchi kama utaratibu unafuatwa.
Kaburu
amesema Simba SC ilikuwa tayari kukaa mezani na Azam kwa mazungumzo, lakini kwa
kuwa Azam haipo tayari kutambua haki za Simba SC na imekuwa ikilitekeleza suala
hili kiholela, hivyo haioni sababu za kuzungumza na Azam FC na kuliacha suala
hili liende kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji kama TFF
ilivyoagiza.