Na Mahmoud Bin Zubeiry |
RATIBA ya michuano ya Afrika mwakani imetoka na mabingwa wa
Tanzania Bara, Simba SC ya Dar es Salaam wataanza na Recreativo de Libolo ya Angola,
katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Februari 17 hadi 19
na kurudiana nayo kati ya Machi 2 na 4, mwakani.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa mwishoni mwa wiki na
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la
Shirikisho, Azam FC, wao wataanza na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Azam mwakani watacheza kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika,
wakati Simba SC ilicheza kwa mara ya kwanza michuano hiyo mwaka 1974.
Miaka ya karibuni matokeo ya klabu za Tanzania yamekuwa si ya
kuridhisha na tulishuhudia mwaka huu katika Ligi ya Mabingwa, Simba SC na Yanga
zikishindwa japo kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo, Yanga ikitolewa na
Zamalek na Simba ikitolewa na Al Ahly Shandy ya Sudan.
Mwaka juzi pia timu zetu hazikufua dafu. Simba, waliocheza
Ligi ya Mabingwa, katika Raundi ya Kwanza waliitoa Elan Mitsoudje ya Comoro kwa
jumla ya mabao 4-2 na Raundi ya Pili wakatolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa jumla ya mabao 6-3.
Hata hivyo, Simba ilirudishwa na CAF mashindanoni baada ya
kushinda rufaa waliyomkatia beki wa Mazembe, Janvier Besala Bokungu, aliyevunja
mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
Simba ilicheza mechi maalum ya mkondo mmoja na Wydad
Casablanca ya Morocco mjini Cairo, kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya
Mabingwa nchini Misri na kufungwa mabao 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16
bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC
kwa mabao 2-1.
Yanga, iliyocheza Kombe la Shirikisho, ilitolewa Raundi ya
Kwanza tu na Dedebit ya Ethiopia kwa kufungwa jumla ya mabao 6-4.
Ukitazama rekodi ya klabu za Tanzania kwenye michuano ya
Afrika, Simba ndiyo klabu yenye rekodi nzuri zaidi katika michuano hiyo, ikiwa
imewahi kufika Fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, kucheza hatua ya makundi ya
Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, wakiwatoa wapinzani wa Yanga mwaka huu,
Zamalek na pia wakati michuano hiyo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika walicheza Nusu
Fainali mwaka 1974.
Yanga wanafuatia rekodi hiyo ya watani wao wa jadi, wakiwa
wamecheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998, na wakati michuano hiyo ikiitwa
Klabu Bingwa Afrika, walicheza Robo Fainali mara mbili 1969 na 1970 na walifika
pia Robo Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 1996.
Ukitazama ratiba ya mwaka huu, hakuna ubishi kwamba Simba na
Azam wamepangiwa timu za kawaida tu kwa viwango vyao, ambazo kama watakuwa na
maandalizi mazuri watavuka mtihani huo.
Lakini pamoja na ukweli huo, Simba na Azam hawatakiwi
kuwadharau wapinzani wao. Wanatakiwa kufanya maandalizi mazuri, ili wawatoe kwa
uhakika.
Angalau Azam wamekwishaanza maandalizi hivi sasa na wako
ziarani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini Simba hadi jana walikuwa
bado hawajaanza mazoezi rasmi.
Labda ni kwa sababu ya mabadiliko ya benchi la ufundi
waliyofanya- lakini ipo haja ya uongozi wa klabu hiyo kufanya kila
kinachowezekana kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa kambini mapema na kujiandaa
vema.
Nasema kujiandaa vema, kwa sababu wachezaji wanatakiwa
kujengwa kikamilifu kuanzia katika nguvu, stamina, pumzi na uwezo wa kuuchezea
mpira- hivi vitu haviwezekani ndani ya wiki mbili.
Maana yake imekuwa kawaida ya timu zetu kukurupuka na kuja
kuanza maandalizi wiki mbili kabla ya mashindano, matokeo yake zikitolewa
visingizio vinakuwa kibao. Watu wamekwishachoka na visingizio na sasa wanataka
matokeo mazuri na ndiyo maana mpendwa wenu, BIN ZUBEIRY nimeona huu
ni wakati mwafaka kukumbushana umuhimu wa maandalizi. Wasalaam.