Na Princess Asia
TIMU ya Mtibwa
Sugar imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai
inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi
Kuu ya Vodacom baada ya leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu) kuzamisha African
Lyon mabao 3-1.
Katika
mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, hadi mapumziko Mtibwa Sugar ilikuwa mbele kwa
bao 1-0 lililofungwa dakika ya 22 na Hillary Kasela. Hassan Kabunda
aliisawazishia African Lyon katika dakika ya 53.
Mabao
mengine ya washindi yalifungwa na Godfrey Mohamed dakika ya 64 na Juma Lazio
akapachika la mwisho dakika ya 87. Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar sasa itacheza
mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Azam ambayo nayo leo asubuhi (Desemba
19 mwaka huu) iliilaza JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa
Chamazi. Bao la Azam lilifungwa dakika ya 46 na Mudathiri Yahya.
Mechi hiyo
ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu) saa 8 kamili
mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Nusu fainali ya
pili nayo itachezwa kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 10 kamili jioni.
Robo fainali
ya tatu kati ya Oljoro JKT na Simba, na robo fainali ya nne zinachezwa leo saa
10 kamili jioni (Desemba 19 mwaka huu) kwenye viwanja vya Karume na Chamazi,
Dar es Salaam.
Mechi ya
fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili (Desemba 23
mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.