Mwaikimba ataendelea kucheka na nyavu leo? |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kinshasa
AZAM FC
inashuka dimbani leo kumenyana na Shark FC katika Nusu Fainali ya Kombe la
Hisani mjini hapa, kwenye Uwanja wa Martyrs.
Awali,
Shirikisho la Soka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), liliitaka Azam FC kucheza
mechi moja zaidi, baada ya kufuzu Nusu Fainali, lakini baada ya majadiliano,
mpango huo umefutwa na leo Wana Lamba Lamba wanacheza Nusu Fainali moja kwa
moja.
Azam iliingia
Nusu Fainali juzi baada ya kuilaza Real de Kinshasa kwenye Uwanja huo huo wa
Martyrs, shukrani kwao, washambuliaji Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah
waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi.
Ikiongezewa
nguvu na nyota wake watatu, Kipre Tchetche, Kipre Balou raia wa Ivory Coast na
Mkenya, Joackins Atudo waliochelewa mechi mbili za awali, Azam juzi ilitawala
mchezo na kama si rafu za wapinzani wao, ingevuna ushindi mtamu.
Hadi
mapumziko, tayari Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na
Mwaikimba dakika ya 21, ambaye aliunganisha pasi nzuri ya Kipre kutoka wingi ya
kushoto.
Hilo lilikuwa
bao la pili kwa Mwaikimba, mshambuliaji wa zamani wa Kahama United, Ashanti
United, Yanga, Prisons na Kagera Sugar katika mechi tatu za mashindano haya
alizocheza, awali alifunga katika sare ya 1-1 na Dragons.
Kipre
Tchetche alilazimika kutoka nje ya Uwanja dakika ya 43 kutokana na rafu za
wachezaji wa Real, nafasi yake ikichukuliwa na Samih Hajji Nuhu.
Real
walikuwa wakipiga kiatu haswa na kiungo Waziri Salum aliungana na Kipre
Tchetche kuuacha Uwanja kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo, ingawa nafasi yake
ilichukuliwa na Uhuru Suleiman dakika ya kwanza ya kipindi cha pili.
Awali ya
hapo, refa Madila Achille alimtoa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43 beki
Muipalayi Igongo kwa kumchezea rafu mbaya Gaudence Mwaikimba, ambayo chupuchupu
naye imtoe nje, kiasi cha kulazimika kumalizia mechi akichechemea.
Kipindi cha
pili, Azam waliendelea kuwafundisha soka Real na katika dakika ya 73, kazi
nzuri ya Mwaikimba ilisaidia kupatikana bao la pili. Mpira mrefu uliopigwa na
kipa Mwadini Ally, Mwaikimba aliumiliki vema, akatoa pasi pembeni kushoto kwa
Hajji Nuhu ambaye aliingia ndani kidogo na kukata krosi maridadi iliyounganishwa
kimiani na Seif.
Humphrey
Mieno alikuwa mwathirika mwingine wa rafu za Real, baada ya kulazimika kutoka
nje dakika ya 77, akimpisha Abdi Kassim ‘Babbi’.
Azam
walionekana kuridhika baada ya kuwa wanaongoza mabao 2-0 na wakafanya uzembe
uliowapa bao la kufutia machozi Real, lililofungwa na Bisole Panzu dakika ya
78.
Katika mechi
zake mbili za awali za Kundi B, Azam ilitoka 1-1 na Dragons na ikafungwa 2-0 na
Shark FC.
Nusu Fainali
nyingine itachezwa kesho wakati Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu
zitachezwa Jumapili na Azam itaondoka hapa Jumatatu kurejea nyumbani.