Azam FC |
Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA wa
Kombe la Hisani la DRC, Azam FC wanatarajiwa kuanza mazoezi leo kwenye Uwanja
wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya
mapumziko mafupi ya sikukuu ya Krisimasi.
Katika maozezi
hayo, wachezaji watatu wa kigeni, beki Joackins Atudo, kiungo Humphrey Mieno wote
wa Wakenya na mshambuliaji Brian Umony wa Uganda hawatakuwapo, kwa sababu bado
wana udhuru hadi baada ya sikukuu ya Krisimasi.
Azam ilitua
Dar es Salaam Jumatatu usiku, ikitokea Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), ilikotwaa Kombe la Hisani, linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la
Soka la DRC.
Azam walitwaa
taji hilo Jumamosi iliyopita, baada ya kuwachapa wenyeji, Dragons FC kwa
penalti 4-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Azam iliingia
fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya DRC
Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
Kikosi cha
Azam kilichoshiriki mashindano hayo ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre
Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki,
Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson Kakolaki,
Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri Salum, Humphrey
Mieno na Joackins Atudo.
Katika
mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake
matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti. Mchezaji mwingine wa kigeni wa Azam,
Brian Umony wa Uganda, atajiunga na timu hiyo baada ya sikukuu pia.
Azam wamepangwa
Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal
Union ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Kundi A lina
timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Michuano ya Kombe
la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya
Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka
ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu
wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Kamati Maalum ya Kusimamaia michuano
hiyo, inaonesha kuwa katika mchezo wa kwanza utakaochezwa siku ya ufunguzi
itakuwa ni kati ya Bandari kutoka Unguja ambayo itacheza na Jamhuri kutoka
kisiwani Pemba ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho
Barani Afrika, pamabanolitakalochezwa katika uwanja wa Mao Tse Tung mjini
Unguja, huku usiku wa siku hiyo hiyo katika Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja
pambano la ufunguzi rasmi katika mashindano hayo likiwakutanisha mabingwa wa
soka nchini Tanzania, Simba SC ambao watapambana na mabingwa wa soka nchini
Kenya, Tusker.
Kwa mujibu
wa ratiba hiyo jumla ya timu nane zitashiriki katika mashindano hayo ambayo
yamejipatia umaarufu mkubwa visiwani hapa, timu hizo zimegawanya katika makundi
mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
Awali
michuano hiyo ilitarajiwa kuanza kisiwani Pemba tarehe 1 Januari, lakini
kutokana na kujitoa katika mashindano kwa klabu ya Al-Ahly ya Misri kutokana na
klie kilichoelezwa sababu za kiusalama, mechi zote sasa zitachezwa kisiwani
Unguja na ufunguzi ukipangwa kuanza tarehe 2 badala ya tarehe 1 januari.
Bingwa wa
michuano hiyo ataondoka na zawadi ya kombe na fedha taslim Tsh.Milioni kumi
(10,000,000), mshindi wa pili Milioni tano (5,000,000), pamoja na zawadi nyengine
ambazo zimegawanywa katika makundi tofauti ikiwemo zawadi ya mfungaji bora,
mchezaji bora, mwamuzi bora, kipa bora, mwandishi wa habari bora, timu bora na
zawadi nyinginezo.