Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Kipingu akimkabidhi nahodha wa timu ya Azam FC, Abdul Mgaya kombe la Ubingwa wa michuano ya Uhai Cup 2012 baada ya timu hiyo kuifunga Coastal Union ya Tanga kwa penalti 3-1 katika mchezo wa fainali ya vijana chini ya miaka 20 uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Katikati ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga. (Picha zote na Habari Msetoto Blog)
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah akimkabidhi zawadi ya mfungaji bora wa mashindano ya vijana chini ya miaka 20 ya Uhai Cup, Ramadhani Mkipalamoto wakati wa fainali ya michuano hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Azam FC wakishangilia baada ya kukabidhiwa kombe lao.
Golikipa wa Azam FC, Aishi Salum akiokoa moja ya hatari zilizoelekezwa langoni mwake.
Mshambuliaji wa Coastal Union, Twaha Shekue akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Azam FC, Samwel Mkomola
Na Prince Akbar
TIMU ya
vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Azam, maarufu kama Azam Academy, imehitimisha
wiki ya furaha kwa klabu hiyo, baada ya kunyakua ubingwa wa Kombe la Uhai, linaloshirikisha
timu za vijana za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo
kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Azam Akademy
imetwaa ubingwa huo, baada ya kushinda kwa penalti 3-1, kufuatia sare ya 2-2 na
Coastal Union ya Tanga ndani ya dakika 120 za pambano kali na la kusisimua.
Ushindi wa
Azam Academy, unakuja siku moja tu baada ya kaka zao, Azam FC kutwaa ubingwa wa
Kombe la Hisani jana mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa
kuwafunga wenyeji Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 90.
Jana Azam
walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha
dakika ya 75 na katika mikwaju ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju
miwili ya Dragons, wakati Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na
Samih Hajji Nuhu walifunga penalti za Azam.
Katika mchezo
wa leo, Azam ilimenyana kiume na Coastal ambayo inaonekana kuinukia vizuri
katika uwekezaji kwenye soka ya vijana kabla ya bingwa kupatikana kwa mikwaju
ya penalti.
Mapema asubuhi
katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Simba waliokuwa mabingwa watetezi, waliifunga
3-0 Mtibwa Sugar na kunyakua nafasi hiyo.
Aidha, Bakari
Shime wa Coastal Union ametwaa tuzo ya Kocha bora, Mansur A. Mansur wa Coastal
Union kipa bora, Ramadhan wa Simba aliyefunga mabao sita, ameibuka mfungaji
bora, Ruvu Shooting timu yenye Nidhamu, Joseph Kimwaga wa Azam mchezaji bora na
Isiaka Mwalile refa bora.