Zanzibar Heroes watang'ara leo? |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
TIMU ya soka
ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes leo inaanza kampeni zake za kuwania Kombe
la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwa kumenyana
na Eritrea katika mchezo wa Kundi C, utakaonza saa 9:00 alasiri Uwanja wa
Mandela, Namboole mjini hapa
Mchezo huo,
utafuatiwa na mchezo mwingine wa kundi hilo, ambao unatarajiwa kuwa mkali zaidi
na wa kusisimua kati ya Rwanda na Malawi kuanzia saa saa 12:00 jioni.
Kikosi cha
Zanzibar Heroes kiliagwa Jumatano visiwani Zanzibar katika Hoteli ya Bwawani ambayo
inamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mgeni rasmi katika hafla hiyo
alikuwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk.
Kikosi
kiliondoka Alhamisi Zanzibar kuaa Kampala kikipitia Dares Salaam na kimeondoka
na msafara wa watu 30, wakiwemo wachezaji 20, benchi la ufundi na viongozi wa
Serikali na Chama cha Soka Visiwani Zanzibar (ZFA).
Hata hivyo,
Heroes itamkosa kiungo wake mahiri Abdulhalim Humud, ambaye ni majeruhi.
Kikosi
kinachotarajiwa kuanza leo Heroes ni; Mwadin Ali Mwadini, Nassor Masoud ‘Cholo’,
Samir Hajji Nuhu, Agrey Moris, Nadir Haroub Ali 'Canavaro, Sabri Ali, Khamis
Mcha 'Vialli', Is-haka Othman, Amir Hamad, Twaha Mohammed na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Tayari mechi
za awali za Kundi A na B zimekwishachezwa na leo Kundi C ndio linafichua makali
yake kwa mara ya kwanza.
Katika mechi
za ufunguzi za Kundi A, Ethiopia waliifunga Sudan Kusini 1-0, wakati Uganda waliichapa
Kenya 1-0 pia juzi, Uwanja wa Mandela, Namboole.
Mechi za Kundi
B jana, Burundi iliitandika Somalia mabao 5-1, kabla ya Tanzania Bara,
Kilimanjaro Stars kuilaza Sudan 2-0.