Cannavaro kushoto akizungumza na Nahodha wa Azam, Aggrey Morris |
Na Mahmoud Zubeiry
WACHEZAJI wa
Yanga SC, wamesema kwamba sasa wanajipanga kwenda kuvunja rekodi ya Coastal
Union kutofungwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani, Mkwakwani, Tanga Jumamosi wiki
hii.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY kwa niaba ya wenzake jana, Nahodha Msaidizi wa Yanga, Nadir
Haroub Ally ‘Cannavaro’ alisema kwamba wanataka kustawisha uongozi wao katika
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuwafunga Coastal Jumamosi.
Alisema
wanajua Coastal ni timu nzuri na wanatarajiwa upinzani katika mechi hiyo, ila
ameonya Yanga ya sasa ni tishio na wachezaji wako vizuri ‘ile mbaya’.
“Kwa kweli
mimi na wachezaji wenzangu tunamshukuru mwalimu mpya (Ernie Brandts) kwa kutupa
vitu vipya na muhimu. Timu yetu imebadilika na kila mtu anaona sasa. Wale
Coastal si hawafungwi kwao wale, sasa sisi tutaenda kuwafunga pale pale, tena
kipigo kikali,”alisema.
Lakini pia
habari za ndani kutoka Yanga zinasema kwamba tayari wachezaji wameahidiwa donge
nono iwapo watashinda mechi hiyo.
Wachezaji
hao, walizawadiwa Sh. Milioni 15 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC juzi
katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Ushindi huo,
uliifanya Yanga iongoze Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 26, ikiwa imebakiza mechi
moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Caostal Union mjini Tanga, ikifuatiwa na
Simba SC yenye pointi 23, ambayo juzi imefungwa 2-0 na Mtibwa Sugar mjini
Morogoro.