Kiiza baada ya kufunga bao la pili |
Kavumbangu wa pili kutoka kushoto, akishangilia bao lake na wenzake |
Kavumbangu wa kwanza kushoto |
Kavumbangu akimfunga kipa wa Azam, Mwadini Ali |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC
imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuifunga Azam
FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo,
unaifanya Yanga iongoze Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 26, ikiwa imebakiza mechi
moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Caostal Union mjini Tanga, ikifuatiwa na
Simba SC yenye pointi 23, ambayo leo imefungwa 2-0 na Mtibwa Sugar mjini
Morogoro.
Hadi
mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji
wa kimataifa wa Burundi, Didier Kvumbangu aliyeunganisha krosi ya Simon Msuva
kutoka wingi ya kulia dakika ya tisa.
Katika
kipindi hicho, Yanga timu zote zilicheza kwa kiwango sawa, isipokuwa Yanga
ndiyo iliyokuwa na mashambulizi ya kutisha zaidi.
Mabeki wa
Yanga walimdhibiti vema mshambuliaji hatari wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’ na
kitendo cha kocha Mholanzi, Ernie Brandts kupanga viungo wawili wakabaji,
Athumani Iddi ‘Chuji’ na Frank Domayo viliisaidia timu hiyo kuwabana Azam katikati
ya Uwanja.
Kipindi cha
pili, Yanga walirudi vizuri zaidi na kuifunika kabisa Azam, ambayo leo hakika
ilimsononesha kocha wake, Muingereza Stewart Hall.
Mganda, Hamisi
Kiiza ‘Diego’ aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 68, akiunganisha krosi ya
Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao
hilo, Kiiza alivua jezi yake na kubaki na fulana ya njano yenye maandishi; Rest
In Peace Mafisango, I miss you So much my brother, maana yake akimuenzi
aliyekuwa kiungo wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango aliyefariki dunia kwa ajali
ya gari Mei mwaka huu akiwa mchezaji wa klabu hiyo.
Kwa ujumla Yanga
imebadilika mno kiuchezaji na sasa wanacheza kwa kuonana, kupeana pasi za
uhakika ndefu na fupi, kuwabana wapinzani na pia bila kuchoka muda wa mchezo.
Kikosi cha Yanga
SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Simon
Msuva/David Luhende, Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbangu.
Azam FC; Mwadini Ally, Erasto Nyoni/Samir
Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris na Said Mourad, Jabir Aziz/Ibrahim
Mwaipopo, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’/Abdi Kassim ‘Babbi’, Salum
Abubakar, John Bocco na Kipre Tcheche.
Katika
mchezo wa utangulizi, Yanga B imewafunga Azam B, maarufu kama Azam Academy
mabao 2-0. Mabao ya Yanga B yalifungwa na Joseph Banda na Claver Charles
kipindi cha kwanza.
Katika mchezo
mwingine wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar iliichapa mabao 2-0 Simba SC, Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro, mabao ya Said
Mkopo na Hussein Javu.
Simba inabaki
na pointi zake 23, baada ya kucheza mechi 12, ikiipisha kileleni Yanga yenye
pointi 26 sasa. Simba itamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kumenyana na
Toto African uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.