// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); WATANO WALIOACHA HISTORIA ISIYOFUTIKA CHALLENGE - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE WATANO WALIOACHA HISTORIA ISIYOFUTIKA CHALLENGE - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Monday, November 19, 2012

    WATANO WALIOACHA HISTORIA ISIYOFUTIKA CHALLENGE

    Bwalya

    KALUSHA BWALYA:
    SAHAU kuhusu Zambia iliyochukua Kombe a Challenge mwaka 2006, wakati huo imekwishajitoa katika nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kuingia nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA).
    Zambia iliyotikisa katika soka ya Afrika Mashariki na kati ni ile iliyokuwa ikiitwa KK Eleven kuanzia miaka ya 1970 hadi 1990 mwanzoni, kabla ya ajali ya ndege iliyoua nyota wa kikosi hicho pwani ya Gabon mwaka 1993.
    Kalusha Bwalya alikuwa katika orodha ya wachezaji waliotakiwa kuingia kwenye ndege iliyopata ajali, lakini bahati nzuri kwake alisema atatokea kwenye klabu yake moja kwa moja Ulaya kwenda Tunisia, hivyo akanusurika.
    Katika historia yake ya ushiriki wa Challenge, KK Eleven ilibeba taji hilo mwaka 1984 na 1991 ambao, Kalusha Bwalya aliungana na Majid Musisi katika ufungaji bora, kila mmoja akifunga mabao yake matatu.
    Challenge ya mwisho kwa Bwalya ilikuwa mwaka 1992 mjini Mwanza, alipoiongoza Zambia hadi Nusu Fainali ilipotolewa na Uganda kwa penalti 4-2, Uwanja wa CCM Kirumba kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
    Huwezi kuizungumzia historia ya Challenge bila ya kumtaja Bwalya, aliyezaliwa Agosti 16, mwaka 1963 mjini Mufulira, kwani enzi zake alikuwa mkali haswa.
    Huyo ni mchezaji aliyeichezea Zambia mechi nyingi zaidi na kuifungia mabao mengi zaidi pia kuliko mchezaji yoyote hadi sasa. Ndiye mchezaji babu kubwa zaidi kuwahi kutokea katika ardhi ya Zambia. Unamzungumzia Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 1988, ambaye mwaka 1996 aliingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, ambayo ilichukuliwa na Mwafrika mwenzake, George Weah.

    Omondi Philip
    PHILIP OMONDI:
    UGANDA ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Challenge, wakiwa wamebeba Kombe hilo mara 12 (1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009 na 2011).
    Wapo wachezaji wawili ambao huwezi kuwatenganisha na mafanikio ya The Cranes katika Challenge. Akina nani hao?
    Wote hawa wamekwishatangulia mbale ya haki hivi sasa, Philip Omondi na Majjid Musisi.
    Phillip Omondi aliyezaliwa mwaka 1957 na kufariki dunia Aprili 21, mwaka 1999 huyu alikuwa mtu hatari sana enzi zake na waliobahatika kumuona wanaweza kukiri juu ya hilo.
    Omondi aliyechezea klabu ya Kampala City Council FC kuanzia mwaka 1973 hadi 1979, alipotimkia Sharjah ya Falme za Kiarabu (UAE) alikuwa shukaa wa Uganda hadi kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
    Omondi aliichezea The Cranes katika fainali za Afrika miaka ya 1974, 1976 na za 1978, ambazo pamoja na kuifikisha Cranes fainali, pia aliibuka mfungaji bora.
    Kwenye Challenge, Omondi aliisaidia mno Uganda kutwaa mataji ya mwaka 1973 na 1977.
    Katika fainali za mwaka 1978, mkali wa mabao wa zamani wa Uganda, Phillip Omondi aliungana na Opoku Afriyie na Segun Odegbami katika ufungaji bora, kila mmoja akipachika nyavuni mabao matatu. Leo Omondi hayupo duniani, lakini huwezi kuzungumzia historia ya Challenge bila kumtaja yeye.

    Musisi
    MAJID MUSISI:
    NI kweli, Philipo Omondi alikuwa noma enzi zake, lakini unaweza kusema nini kuhusu Majid Musisi Mukiibi?
    Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Septemba 15, mwaka 1967 kabla ya kufariki dunia Decemba 13, mwaka 2005 vyombo vya habari Uganda vimechekecha vikaamua kuweka bayana, huyo ndiye mchezaji bora zaidi kihistoria kuwahi kutokea nchini humo.
    Musisi, ambaye ni mchezaji wa kwanza wa Uganda kucheza soka ya kulipwa Ulaya, alikuwa ana majina mawili maarufu ya utani enzi zake, ambayo ni Tyson na Magic. Tyson kwa sababu alikuwa mkorofi na Magic ni kwamba soka yake iliitwa ya miujiza.
    Huyo aliisaidia The Cranes kutwaa Kombe la Challenge katika miaka ya 1989 na 1990. Mfumo wa maisha ya kuendekeza pombe, ulimfanya afananishwe na magwiji wa soka duniani akina George Best, Eric Cantona au Paul Gascoigne ‘Gazza’.
    Musisi alikuwa ana utajiri miguuni mwake na mabeki kwa pamoja na makipa walikuwa wanamheshimu sana mtu huyo. Alikuwa hashindwi kufanya jambo anapoamua kufanya kwa juhudi zake zote.
    Umaarufu wake uliwavutia vijana wengi kucheza soka Uganda na Afrika Mashariki kwa ujumla. Jamaa alikuwa anaijua soka.

    Nteze John
    NTEZE JOHN:
    WENGINE wanaweza kujiuliza kwa nini siyo Sunday Manara ama Zamoyoni Mogella, Peter Tino au Edibily Lunyamila, lakini jibu ni kwamba, wote hao hawafui dafu mbele ya Nteze John Lungu kwa kufanya vitu vikubwa kwenye Kombe la Challenge.
    Haimaanishi Nteze alikuwa anawazidi kisoka akina Abdallah Kibadeni, Mogella, Lunyamila, Said Mwamba Kizota na wengine waliowahi kuwika katika soka ya Tanzania, la hasha- ila Nteze aling’ara zaidi yao kwenye michuano hiyo.
    Huyo ndiye aliyekuwa shujaa wetu wakati tunachukua taji la pili la michuano hiyo, mwaka 1994 mjini Nairobi, Kenya.
    Mabao yake manne aliyofunga katika Kundi A, kwenye michuano hiyo yaliifanya Tanzania Bara iongoze kundi hilo kwa pointi tisa ilizokusanya kutoka na kushinda mechi zote za kundi lake, Nteze akifunga katika kila mechi.
    Novemba 29, Tanzania ikiitandika Somalia mabao 4-0, Nteze alifunga mabao mawili katika dakika za 11 na 84, mengine yakifungwa na George Masatu dakika ya 67 na Madaraka Suleiman dakika ya 74.
    Siku mbili baadaye Nteze alifunga bao pekee la ushindi dakika ya 57, Bara ikiwafunga wenyeji Kenya 1-0, wakati Desemba 3, Bara ikiichapa Djibouti 3-0, Nteze alifunga la tatu dakika ya 75, baada ya Edward Chumila (sasa marehemu) kufunga dakika ya pili na Clement Kahabuka dakika ya 30.
    Nteze hakufunga katika mechi mbili zilizofuata, Nusu Fainali dhidi ya Eritrea, bao pekee la Said Mwamba ‘Kizota’ dakika ya saba likiipa Bara ushindi wa 1-0 na fainali, ambayo baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 120 dhidi ya Uganda, Bara ilifanikiwa kutwaa Kombe kwa mikwaju ya penalti 4-3.
    Ilikuwa ni Desemba 10, wakati mabao ya Stars yalipotiwa kimiani na Juma Amir Maftah dakika ya 14 na Kizota dakika ya 40 wakati Iddi Batambuze aliifungia Uganda dakika ya 47 kabla ya George Ssemogerere dakika ya 88 kusawazisha.
    Nteze aliibuka pia mfungaji bora wa michuano hiyo kwa mabao yake manne na kutwaa Kiatu cha Dhahabu.

    Oliech
    DENNIS OLIECH:
    WAMETOKEA wanasoka wengi Kenya ambao waling’ara kwenye Challenge, lakini kama ilivyo kwa wachezaji wa Tanzania unahitajika utulivu wa hali ya juu, ili kumtaja mmoja ambaye daima anastahili kukumbukwa katika historia ya michuano hiyo. 
    Mfungaji wa bao la tatu na la ushindi katika dakika ya 72 ya fainali ya Kombe la Challenge Desemba 14, mwaka 2002 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Tanzania Bara ikilala 3-2 na kupoteza matumaini ya kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu.
    Nani zaidi ya Dennis Oliech. Na kwa nini asahaulike mtu huyo siyo tu kwa kuwakomoa wenyeji na kuwapokonya tonge mdomoni, bali soka yake iliyomuuza Ulaya baadaye.
    Siku hiyo, Emmanuel Gabriel alitangulia kuifungia Bara dakika ya 28, kabla ya Paul Oyuga kusawazisha dakika ya 30 na Mecky Mexime kufunga la pili kwa penalti dakika ya 59 na John Barasa kuisawazishia Harambee Stars dakika ya 70 na Oliech kupiga la ushindi dakika ya 72.
    Oliech alikuwa mfungaji bora katika fainali hizo kutokana na mabao yake matano, akiwa ana umri wa miaka 17 tu wakati huo.
    Oliech alizaliwa Februari 2, mwaka 1985, baada ya kung’ara kwenye fainali hizo, mwaka 2003 alinunuliwa na Al-Arabi ya Qatar hadi mwaka 2005, aliposaini mkataba wa miaka minne na  FC Nantes ya Ufaransa na kuanza safari yake kuogelea kwenye bwala la fedha Ulaya na sasa anachezea Auxerre.
    Aliiwezesha Kenya kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 na alicheza vizuri kwenye fainali hizo nchini Tunisia na mwaka huo huo akatabiriwa kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari baadaye duniani, akiwekwa katika orodha moja na Wayne Rooney wa Manchester United. Oliech kwa sasa ameipa kisogo michuano ya Challenge, ingawa bado anaichezea Harambee Stars katika michuano mikubwa, ila Challenge ndio iliyomtoa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WATANO WALIOACHA HISTORIA ISIYOFUTIKA CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top