Bin Kleb kushoto akiingia kwenye vyumba vya wachezaji wakati wa mapumziko jana. Mbele yake ni Seif Ahmad Magari |
Mosha katikati akiingia kwenye vyumba vya wachezaji wakati wa mapumziko jana |
Na Mahmoud Zubeiry
WACHEZAJI wa
Yanga SC, wamezawadiwa Sh. Milioni 15 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC
jana katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Ushindi huo,
umeifanya Yanga iongoze Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 26, ikiwa imebakiza mechi
moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Caostal Union mjini Tanga, ikifuatiwa na
Simba SC yenye pointi 23, ambayo jana imefungwa 2-0 na Mtibwa Sugar mjini
Morogoro.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb aliiambia BIN ZUBEIRY jana
kwamba, waliwapa wachezaji wao ahadi hiyo kabla ya mechi na wameitekeleza baada
ya mechi.
Aidha, Bin
Kleb alisema kwamba wamemrejesha kundini Yanga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu
hiyo, Davis Mosha ambaye ametoa mchango mkubwa katika ushindi wa jana.
“Ushindi wa leo
(jana), Mosha ana mchango mkubwa sana, tumemrejesha kundini na tunapenda wana
Yanga wote kuanzia sasa wajue Mosha tuko naye tena na yuko nasi bega kwa bega
katika kuhakikisha Yanga inarejesha heshima,”alisema Bin Kleb.
Hadi
mapumziko jana, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na
mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kvumbangu aliyeunganisha krosi ya
Simon Msuva kutoka wingi ya kulia dakika ya tisa.
Katika
kipindi hicho, Yanga timu zote zilicheza kwa kiwango sawa, isipokuwa Yanga
ndiyo iliyokuwa na mashambulizi ya kutisha zaidi.
Mabeki wa
Yanga walimdhibiti vema mshambuliaji hatari wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’ na
kitendo cha kocha Mholanzi, Ernie Brandts kupanga viungo wawili wakabaji,
Athumani Iddi ‘Chuji’ na Frank Domayo viliisaidia timu hiyo kuwabana Azam katikati
ya Uwanja.
Kipindi cha
pili, Yanga walirudi vizuri zaidi na kuifunika kabisa Azam, ambayo leo hakika
ilimsononesha kocha wake, Muingereza Stewart Hall.
Mganda, Hamisi
Kiiza ‘Diego’ aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 68, akiunganisha krosi ya
Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao
hilo, Kiiza alivua jezi yake na kubaki na fulana ya njano yenye maandishi; Rest
In Peace Mafisango, I miss you brother, maana yake akimuenzi aliyekuwa kiungo
wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Mei
mwaka huu akiwa mchezaji wa klabu hiyo.
Kwa ujumla
Yanga imebadilika mno kiuchezaji na sasa wanacheza kwa kuonana, kupeana pasi za
uhakika ndefu na fupi, kuwabana wapinzani na pia bila kuchoka muda wa mchezo.
Kikosi cha Yanga
SC jana kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Simon
Msuva/Paul Ngalema, Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbangu.
Azam FC; Mwadini Ally, Erasto Nyoni/Samir
Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris na Said Mourad, Jabir Aziz/Ibrahim
Mwaipopo, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’/Abdi Kassim ‘Babbi’, Salum
Abubakar, John Bocco na Kipre Tcheche.
Katika
mchezo wa utangulizi, Yanga B imewafunga Azam B, maarufu kama Azam Academy
mabao 2-0. Mabao ya Yanga B yalifungwa na Joseph Banda na Claver Charles
kipindi cha kwanza.