Brandts akiwa Uwanja wa Chamazi mida hii |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC leo imeingia kambini katika hoteli ya Kiromo,
Bagamoyo mkoani Pwani kujiandaa na mchezo wake wa Jumapili wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa kawaida, Yanga huweka kambi Bagamoyo katikati ya Ligi,
inapokuwa inajiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC hivyo
kwa kwenda huko kuweka kujiandaa na mchezo huo, maana yake wanaupa uzito sawa
na pambano la watani.
Wakati vijana wa Yanga wakiwa Bagamoyo, Kocha Mkuu wa klabu
hiyo, Mholanzi Ernie Brandts yupo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi,
akiwafanyia ‘ushushushu’ wapinzani wake hao wanaomenyana na Coastal Union ya
Tanga mida hii, kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza 3-0.
Brandts jana aliiongoza Yanga SC kuendeleza wimbi la ushindi
katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa Mgambo JKT ya
Handeni, Tanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Yanga sasa iwe na pointi sawa na
mabingwa watetezi, Simba SC waliotoa sare ya 1-1 na Polisi mjini Morogoro leo,
ingawa inazidiwa bao moja tu katika wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0,
yaliyotiwa kimiani na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Didier
Kavumbangu.
Cannavaro alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Oscar
Joshua dakika ya pili kutoka wingi ya kulia, wakati Kavumbangu alimalizia pasi
ya Hamisi Kiiza dakika ya 39.
Pamoja na kutoka uwanjani wamelowa kipindi cha kwanza, lakini
Mgambo JKT walicheza soka ya kuvutia na mara mbili walikaribia kufunga kupitia
kwa Juma Mwinyimvua.
Yanga walicheza vema dakika 45 za kipindi cha kwanza, tofauti
sana na mechi za awali ambazo wamekuwa ‘wakichezewa’ sana na wapinzani.
Ilishuhudiwa katika kipindi hicho, Yanga wakimiliki zaidi
mpira na kupeana pasi za uhakika, ingawa mashambulizi yao mengi walipitisha
pembeni, hasa upande wa kulia.
Hamisi Kiiza, Msuva na Kavumbangu walicheza kwa uelewano
mkubwa pale mbele na kulitia misukosuko haswa lango la Mgambo.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto wao tena na
kuendelea kuwachachafya Mgambo.
Hata hivyo, iliwachukua Yanga dakika 34 kupata bao la tatu,
mfungaji akiwa ni Jerry Tegete aliyeingia dakika ya 68 kuchukua nafasi ya
Kavumbangu.
Tegete alifunga bao hilo akiunganisha krosi maridadi ya beki
wa kushoto, Oscar Joshua.
Pamoja na kufungwa, Mgambo waliendelea kusukuma mashambulizi
langoni mwa Yanga, ingawa leo mabeki wa timu hiyo, inayofundishwa na Mholanzi,
Ernie Brandts walicheza kwa uelewano mkubwa na kudhibiti hatari zote langoni
mwao.
Mgambo inayofundishwa na Mohamed Kampira, ilipata pigo dakika
ya 85, baada ya beki wake wa kulia, Salum Mlima kutolewa kwa kadi nyekundu ya
moja kwa moja kwa kumchezea rafu mbaya Mbuyu Twite.