INADAIWA Nahodha
wa Simba, Juma Kaseja ameamua kuachana na timu hiyo na tayari amewaaga wachezaji
wenzake na kuwaambia yeye na klabu hiyo basi.
Kwa mujibu
wa wachezaji wenzake, Kaseja ameamua Simba basi, baada ya kuumizwa kwa jinsi
alivyodhalilishwa na mashabiki Jumamosi Morogoro.
Na Mahmoud Zubeiry |
“Juma hapa
ndio basi kaka, Kasema yeye na Simba basi, amesononeshwa mno na jinsi
alivyodhalilishwa baada ya mechi ya Morogoro,”alisema mchezaji mmoja wa Simba
baada ya mazoezi ya timu hiyo Uwanja wa Kinesi jana.
Kaseja
alitukanwa na kutishiwa maisha na mashabiki wa Simba baada ya mechi dhidi ya Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro wakimtuhumu kufungwa mabao ya kizembe.
Ezekiel Kamagwa,
Ofisa Habari wa Simba, ni rafiki yangu, na tumesoma naye shule moja licha ya
kufanya naye kazi ofisi moja pia, alinisimulia tukio la Kaseja kuanzia Morogoro
uwanjani, hadi kwenye basi njiani akaniambia alilia baada ya kuona aliyokuwa
akifanyiwa Kaseja.
Kwa kifupi,
Kamwaga alisema Kaseja alitukanwa yeye, familia yake hadi na mama yake na pia
akatishiwa maisha.
Kisa,
kufungwa kwenye mechi na Mtibwa mabao mawili. Najaribu kujiuliza Icer Casillas,
aliyefungwa mabao sita Real Madrid ikichapwa na Barcelona nchini Hispania kwa
nini hadi leo ni kipa namba moja wa klabu hiyo na anaheshimika kwa kiasi kikubwa,
ikiwa Kaseja anasulubiwa kwa kipigo cha Mtibwa?
Sahau kuhusu
yote, huyo ni binadamu kama binadamu wengine wote, kukosea si ajabu, lakini hiyo
siyo hukumu ya kumpa.
Simba ina
benchi la ufundi, na hapana shaka limeyaona mapungufu ya Kaseja hivyo kama kuna
umuhimu wa mabadiliko yatafanywa, ila si mashabiki kwenda kumdhalilisha kama
walivyofanya.
Wanapata wapi
ujasiri huo na hiyo ni tabia gani ya kishenzi? Lakini tujiulize, hawa ni
mashabiki wa kawaida tu au wana ajenda zao nyingine?
Nastaajabu sana
viongozi wa siku hizi wa soka katika nchi hii, wanachezewa hadi barazani kwao. Wanatiwa
vidole mpaka sehemu za hatari na watu ambao wanadhibitika, tena kwa urahisi
sana.
Watu waliomfanyia
fujo Kaseja hawakuwa wakazi wa Morogoro, ni watu ambao walitoka Dar es Salaam
kwenda Morogoro kushuhudia mechi. Ni watu ambao naamini kabisa tunawajua na
tuna uwezo wa kuwachukulia hatua, tukiamua- ili liwe fundisho kwa wajinga wengine.
Watu wakishakuwa
kwenye macho ya watu wengi wanakuwa na ujasiri wa kufanya lolote, kwa sababu
wanajua hakuna watakachofanywa. Lakini tunalea maradhi mabaya sana.
Yule aliyekuwa
Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Nchunga alivamiwa hadi nyumbani kwake na
mashabiki, lakini taarifa ikasema watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi. Tunajua
ukweli, lakini kwa kuwa tumeridhika na tumeona hiyo ndiyo staili ya maisha ya
soka ya Tanzania, tunachukulia poa tu.
Hawa watu
sasa wanatukana, wanadhalilisha, ila kwa sababu naamini wanadekezwa, ipo siku
watakuja kupiga hadi kuua. Kutoka hapo, kama ambavyo ilivyo desturi ya nchi yetu,
tahadhari huchukuliwa baada ya hatari, basi ndipo hatua itachukuliwa.
Kamwaga ananiambia
wale wajinga walipaki gari lao karibu na basi la Simba likiwa njiani kurejea
Dar es Salaam wakataka kumtoa Kaseja kwenye basi wampige na baada ya kumkosa,
hasira zao zikaishia kumtukana.
Nilistaajabu
sana, hao watu walifika Dar es Salaam salama, na kama ni hivyo kesho watashindwa
nini kumfanyia hivyo na Shomari Kapombe au Mwinyi Kazimoto?
Viongozi waliokuwa
katika msafara wa Simba walishindwaje kutoa taarifa Polisi ili msafara wa watu
hao waliofanya ushenzi huo ukamatwe na wahusika wachukuliwe hatua? Tunalea maradhi.
Na kama
kweli tumeamua kulea maradhi, basi tusubiri maafa yakitokea ndipo tutachukua
hatua. Nashangaa sana, viongozi wa klabu zetu na soka Tanzania kwa ujumla kama
hawawezi hata haya mambo madogo madogo, sasa tutarajie wataweza nini?
Namheshimu sana
Juma Kaseja, kama mmoja wa makipa bora waliowahi kutokea Tanzania na ningependa
ajue, yanayomtokea yeye sasa yalimtokea pia hata Athumani Mambosasa na Mwameja
Mohamed, makipa wengine bora kabla yake pale Simba na Tanzania kwa ujumla.
Mambosasa na
Mwameja nao, baada ya kuitumikia Simba vizuri na kuipa heshima kubwa,
hawakuagwa vizuri, walidhalilishwa hivyo kwa kuambiwa wamefungisha na kufanyiwa
udhalili.
Hii ni
desturi ambayo tunailea miaka nenda, rudi sasa, ila naamini iko siku italeta
maafa makubwa, iwapo hatua hazitachukuliwa, kwa sababu wahenga walisema mtoto umleavyo
ndivyo akuavyo na kama hatuwezi kumkunja samaki mbichi, sijui itakuwaje hapo baadaye.
Alamsiki.