13 Novemba, 2012 - Saa 14:42 GMT
Patrick Viera amesema anataka kocha wa Manchester City, Roberto Mancini kusalia katika klabu hiyo, ili kuiongoza kushinda medali zaidi.
Mancini alisaini mkataba mpya na klabu hiyo mwezi Julai mwaka huu, baada ya kuiongoza kushinda kombe la ligi kuu ya Premier msimu uliopita, lakini katika siku za hivi karibuni kumekuwa na fununu kuhusu hatma ya kocha huyo.
Vieira, ambaye ni afisa mkuu anayehusika na masuala ya uendelevu wa soka katika klabu hiyo, amesema Mancini, alisaini mkataba wa miaka mitano na hiyo ni ishara kuwa ana imani na klabu ya Manchester City.
Mancini, mwenye umri wa miaka 47, ni kocha wa Manchester City aliyetia for a zaidi katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kuiongoza kushinda kombe la ligi kuu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 44, mwaka mmoja tu, baada ya kuongoza klabu hiyo kushinda kombe la kwanza la FA.
Lakini mapema mwezi huu, kocha huyo alidokeza kuwa, nusura akihame klabu hiyo mwisho wa msimu uliopita, akisema vilabu kadhaa vilikuwa vimeonyesha nia ya kutaka kumsajili, lakini akaamua kusalia na mabingwa hao wa England.
Licha ya kuwa Manchester City imo alama mbili nyuma na viongozi wa ligi kwa sasa Manchester United, klabu ya Manchester City imeandikisha matokeo mabaya katika michuana na kuwania kombe la klabu bingwa barani ulaya, hali ambayo imesababisha wakosoaji wengi kuhoji kuwepo kwake kama meneja.
IMEHAMISHWA kutoka bb swahili