Vialli akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza jana |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
KIUNGO wa
Zanzibar, Khamis Mcha ‘Vialli’ amesema kwamba pamoja na kufunga mabao mawili
jana, akiiwezesha timu yake kuilaza Rwanda 2-1 na kupanda kileleni mwa Kundi C,
lakini hatakuwa na tamaa na tuzo ya ufungaji bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, bali ataweka mbele maslahi ya timu.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, Vialli alisema
kwamba ikitokea nafasi ya kufunga atafanya hivyo, lakini kama wenzake watakuwa
kwenye nafasi nzuri, atawapasia.
“Ushindi wa
leo ni matunda ya ushirikiano baina yetu kama timu nasi hatuna budi kuendeleza
ushirikiano huu, kwa kuweka mbele maslahi ya timu,”alisema Vialli.
Vialli jana
aliifungIa mabao mawili Zanzibar Heroes, katika mchezo wa Kundi C, Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge uliofanyika kwenye
Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
Kwa ushindi
huo, Zanzibar Heroes imefufua matumaini ya kwenda Robo Fainali ya michuano hii,
ikipanda kileleni mwa Kundi hilo, kwa pointi zake nne, Rwanda ikishuka nafasi
ya pili kwa pointi zake tatu, sawa na Malawi, wakati Eritrea inashika mkia kwa
pointi yake moja.
Vialli
alifunga mabao yake moja kila kipindi, la kwanza dakika ya sita na la pili
dakika ya 61, yote akionyesha yeye ni fundi na mwenye akili na maarifa ya soka
kutokana na kutulia na kumtungua kipa hodari kabisa katika ukanda huu, Jean
Claude Ndoli.
Rwanda
ilipata bao lake kupitia kwa Dadi Birori dakika ya 79, ambaye aliingia uwanjani
dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Tumaine Ntamuhanga.
Mchezo wa jana
kama ulivyokuwa mchezo wa kwanza kati ya Malawi na Eritrea ulitibuliwa na mvua
iliyoharibu mandhari ya Uwanja wa Mandela, hivyo haikuwa wa ufundi zaidi ya
‘butua butua’.
Nahodha wa
Zanzibar, Nadir Heroub ‘Cannavaro’ alisema baada ya mechi hiyo kwamba wamefuta
makosa yao ya mchezo wa kwanza na sasa Wazanzibari wasubiri Kombe, wakati
Haruna Niyonzima wa Rwanda, alilalamikia Uwanja mbovu leo kuwasababisha kucheza
ovyo.