Kizito akishangilia baada ya kufunga usiku huu Uwanja wa Mandela. Kushoto ni Hamisi Kiiza akimkimbilia kumpongeza |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
WENYEJI
Uganda, The Cranes wameanza vema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kuilaza Kenya, Harambee
Stars bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mandela, uliopo Namboole, Kampala, Uganda.
Shukrani kwake,
mshambuliaji wa Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, Geoffrey Kizito aliyefunga bao
hilo pekee la ushindi dakika ya 74, akiunganisha krosi ya Iguma Dennis.
Kwa ushindi
huo, Korongo wa Kampala anafungana na Ethiopia kuongoza Kundi A, kwa pointi
zake tatu kila timu.
Hadi mapumziko
hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na timu zote zilishambuliana
kwa zamu.
Kenya walianza
kwa kasi kwa dakika tano wakicheza soka iliyowasisimua mashabiki wake wachache
waliokuwapo uwanjani, lakini Uganda wakazinduka nao na kuanza kuwapa raha
mashabiki wao kwa soka safi.
Mchezo uliendelea
kuwa hivyo kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, kila upande wakicheza kwa
kujiamini.
Lakini sifa
ziende kwa safu zote mbili za ulinzi kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya
juu.
Kipindi cha
pili timu hizo ziliporejea uwanjani, zililazimika kusimama kwa takriban dakika saba
baada ya taa za uwanjani kuzimika na baada ya mafundi kutatua tatizo hilo,
ndipo kabumbu likaanza tena.
Michuno hiyo
itaendelea kesho kwa mechi mbili, Burundi na Somalia saa 10:00 jioni na baadaye
Tanzania Bara na Sudan saa 12:00 jioni.
Uganda; Abel Dhaira/Hamza Muwonge, Iguma
Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi, Isaac isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey
Kizito, Moses Oloya, Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
Kenya; Duncan Ochieng, Anthony Kimani,
Abdallah Juma, Jockins Atudo, David Owino, David Ochieng, Lama Salim Mohamed, Bernard
Wanyama, Humphrey Mieno, Anthony ‘Muki’ Kimani/Enock Obiero na Clifton Miheso/Paul
Were.