Na Prince Akbar
MZUNGUKO wa
pili wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara huko mashakani kufanyika baada ya
Mapato ya Taifa(TRA) kuzifunga akaunti za udhamini wa ligi hiyo.
TRA
ilizifunga akaunti za TFF ikiwemo ya udhamini wa ligi hiyo ikiwa ni sehemu ya
kulishinikiza Shirikisho la Soka nchini(TFF) kulipa makato ya kodi kwenye
mishahara ya timu ya taifa(Taifa Stars) tokea kipindi cha kocha Marcio Maximo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini(TFF)
Sunday Kayuni alisema mishahara ya makocha wa Taifa Stars tangia kocha Marcio
Maximo ilikuwa haikatwi kodi na hivyo kufanya gharama wanazodaiwa na mamlaka ya
Mapato kufikia shilingi milioni 157,407.968.00.
Alisema
wamekuwa wakipata taarifa ya mara kwa mara toka TRA ikiwakumbusha juu ya makato
hao na wao kuwajibu kuwa hawahusiki kwenye malipo ya mishahara ya makocha hao
kwani ni waajiriwa wa Serikali.
Kayuni
alisema hata hivyo kwa kuwa wao ndio walezi wa makocha hao TRA imeamua
kuzifunga akaunti zao ikiwemo ya udhamini wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara
ambayo ina zaidi ya shilingi milioni 300.
Alisema
kutokana na hali hiyo walifanya mazungumzo ya mara kwa mara na TRA bila ya
mafanikio na kuamua kuunda kamati itayoshirikisha Kamati ya Ligi ikishirikiana
na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kwa ajili ya kufanya
mazungumzo na mamlaka hiyo ya mapato nchini.
“Tunaona
labda tukiunganisha nguvu zetu labda wenzetu wa TRA wanaweza kutusikiliza,
hivyo Kamati tutakayounda kwa kushirikiana na wizara itakwenda kujaribu kufanya
tena mazungumzo na TRA.”alisema Kayuni.
Kwenye
Mkutano huo na waandishi wa habari Kayuni aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Ligi Kuu Saidi Mohamedi na Mkurugenzi Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya
Tanzania Bara Silas Mwakibinga, ambao wote walionyesha umuhimu wa kuunganisha
nguvu zao kuishawishi TRA.