Toto African |
Na Mahmoud Zubeiry
TIMU ya Toto African imejichimbia eneo la Tandika mjini Dar
es Salaam kwa takriban wiki nzima, ikijifua vikali tayari kwa mchezo wao dhidi
ya Simba kesho.
Kocha wa Toto, John Tegete aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba,
yeye hatakuja Dar es Salaam kuungana na timu yake kwa ajili ya mechi hiyo kwa
sababu ya majukumu ya kitaifa, lakini kikosi kipo vizuri.
“Mimi nina majukumu ya maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa Taifa
Stars na Kenya huku Mwanza, ila kila kitu kipo sawa, timu iko huko, imeweka
kambi Tandika na Jumamosi Mnyama anachinjwa Uwanja wa Taifa,”alisema Tegete.
Tegete alisema Toto wafufuliwe kwa kaburini, kwa Simba
watacheza mechi na kushinda kwa sababu wanaamini hao ni vibonde wao tu.
“Na ndiyo maana sina wasiwasi nimebaki Mwanza najua tu vijana
wangu watachinja Mnyama,”alisema.
Toto imekuwa na rekodi ya kuisumbua Simba katika Ligi Kuu
hata ikiwa vibaya na hilo ndilo linatarajiwa kwenye mchezo wa kesho Uwanja wa
Taifa.
Awali, Simba ilitishia kugoma kucheza mechi hiyo kesho, siku
tofauti na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mapema wiki hii limetangaza
kuzirudisha nyuma kwa siku moja mechi zote za mwisho za mzunguko wa kwanza wa
Ligi Kuu, kutoka Jumapili wiki hii hadi Jumamosi, kasoro mechi ya Yanga na
Coastal Union pekee, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Na sababu za kutorudishwa nyuma kwa mechi ya Yanga ni kwa
kuwa Jumamosi kutakuwa na mchezo mwingine wa ligi hiyo, Uwanja wa Mkwakwani,
kati ya Mgambo JKT na Azam FC.
Lakini Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga aliiambia BIN
ZUBEIRY juzi kwamba hawako tayari kucheza siku tofauti na Yanga kwa
sababu ya upinzani uliopo baina yao katika mbio za ubingwa, kwani wanahofia
mchezo mchafu.
“Unajua bwana ligi hii ilipofikia ni pabaya, haiwezekani
uzichezeshe Simba na Yanga siku tofauti, hivyo sisi tunawaandikia barua TFF
kuwataarifu kwamba hatuko tayari kwa mabadiliko hayo,”alisema Kamwaga.
Lakini inavyoonekana Wekundu hao wa Msimbazi wamefyata mkia
na kesho wataingiza timu Taifa.
Mechi nyingine za Jumamosi ni Mgambo JKT na Azam FC Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga, African Lyon na Mtibwa Sugar Chamazi, Dar es Salaam, Prisons
na JKT Ruvu Sokoine, Mbeya, Kagera Sugar na Polisi Morogoro, Kaitaba, Bukoba na
JKT Oljoro na Ruvu Shooting Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.