Na Prince Akbar
SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko ya viingilio vya mechi ya raundi ya
mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana chini
ya umri chini ya miaka 17 kati ya wenyeji, Serengeti Boys na Kongo Brazzaville
itakayochezwa Jumapili wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari
wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo amesema leo kwamba awali kiingilio cha juu
katika mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni kilikuwa Sh. 5,000, lakini kwa
lengo la kuwafanya wadau wa kiingilio hicho kuchangia gharama za mechi hiyo
sasa kutakuwa na viingilio vitatu tofauti katika viti vya VIP.
Wambura amesema
VIP A ambayo ina viti 748 kiingilio kitakuwa sh. 10,000, VIP B inayochukua
watazamaji 4,160 kiingilio ni sh. 5,000 wakati VIP C yenye viti 4,060 kiingilio
ni sh. 2,000. Kwa sehemu nyingine (viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu)
ambavyo jumla yake ni 48,590 kiingilio kitabaki kuwa sh. 1,000.
Amesema Kongo
Brazzaville inatarajia kuwasili leo kwa ndege ya Ethiopian Airlines na itafikia
katika hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo, Dar es Salaam.
Wakati huo
huo, Kamati ya kusaidia Serengeti Boys ishinde, chini ya Mwenyekiti wake,
Ridhiwani Jakaya Kikwete, itakutana na Waandishi wa Habari kesho Saa 5:00
asubuhi katika hoteli ya JB Belmont, ukumbi wa Ngorongoro, Dar es Salaam.