Taifa Stars |
Na Mahmoud Zubeiry
TIMU ya soka
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba, Mwanza kumenyana na Kenya, Harambee Stars katika mchezo wa kirafiki,
ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Tanzania
inakutana na Kenya, zikiwa hazitofautiani sana kwa sasa, japokuwa Harambee inajivunia
wachezaji kadhaa wanaocheza soka ya ushindani Ulaya.
Taifa Stars,
inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen, aliyeanza kazi Mei mwaka huu, akirithi
mikoba ya Jan Borge Poulsen kutoka Denmark pia, haijashinda mechi yeyote tangu
iifunge Gambia 2-1 Juni 10, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika
mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014
Brazil.
Chini ya Kim,
aliyepandishwa kutoka timu za vijana za Tanzania, kazi aliyoanza Aprili mwaka
jana, ilitoka sare ya 1-1 Juni 17, ilitolewa na Msumbji kwa mikwaju ya penalti katika
mchezo wa kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika
Kusini, kufuatia sare ya jumla ya 2-2.
Ilijitupa
uwanjani mara ya mwisho, katika mchezo wa kirafiki, Agosti 15, mwaka huu mjini
Gaborone na kulazimishwa sare ya kufungana mabao 3-3, tena ikitoka nyuma na
kusawazisha.
Kenya
inayofundishwa na Mfaransa Henri Michel, mara ya mwisho kushinda mechi ilikuwa
ni Julai 12, mwaka huu ilipoichapa Botswana nyumbani kwake, Gaborone, mabao
3-1, lakini Harambee Stars katika mechi yao ya mwisho waliyocheza, walifungwa
2-1 nyumbani na Afrika Kusini Oktoba 16, mwaka huu, huo ukiwa mchezo wa
kirafiki.
Mchezo huo,
unatarajiwa kuinufaisha zaidi timu ya Bara, Kilimanjaro Stars, yenye wachezaji
wengi kwenye kikosi hicho, kwani baada ya hapo itaingia kambini kujiandaa na
michuano ya Tusker Challenge 2012, itakayofanyika mjini Kampala, Uganda
mwishoni mwa mwezi huu. Kenya pia itashiriki michuano hiyo ya Challenge.
Wakati Kenya
iliwasili Mwanza jana, Tanzania walianza kujikusanya kambini Jumapili na hadi
kufikia juzi kikosi kilikuwa kimekwishakamilika.
Wachezaji
walioitwa kwa ajili ya mechi hiyo ni makipa Juma Kaseja (Simba SC) na
Deogratius Mushi ‘Dida’ wa Azam FC.
Mabeki;
Kevin Yondan (Yanga), Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam FC), Issa Rashid
(Mtibwa Sugar), Nassoro Masoud ‘Cholo’, Shomari Kapombe na Amir Maftah (Simba).
Viungo;
Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam FC), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan
Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa (Simba), Athuman Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo
(Yanga) na Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji;
John Bocco ‘Adebayor’ (Azam FC), Simon Msuva (Yanga), Christopher Edward
(Simba), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa (TPM, DRC).
REKODI YA STARS MWAKA HUU NA RATIBA
YA MECHI ZIJAZO:
Februari 23, 2012
Tanzania 0 – 0 DRC (Kirafiki)
Februari 29, 2012
Tanzania 1 – 1 Msumbiji (Kufuzu Mataifa ya Afrika)
Mei 26, 2012
Tanzania 0 – 0 Malawi
Juni 2, 2012
Ivory Coast
2 – 0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 10, 2012
Tanzania 2 – 1 Gambia (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 17, 2012
Msumbiji 1 –
1 Tanzania (Tanzania ilitolewa kwa
penalti kufuzu Mataifa ya Afrika)
Agosti 15, 2012
Botswana 3 –
3 Tanzania (Kirafiki)
Novemba 14, 2012
Tanzania Vs Kenya
(Kirafiki)
Machi 22, 2013
Tanzania Vs Morocco (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 7, 2013
Morocco Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
Juni 14, 2013
Tanzania Vs Ivory Coast (Kufuzu
Kombe la Dunia)
Septemba 6, 2013
Gambia Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)