Feliux Sunzu akitibiwa |
Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. ataongezewa mkataba baada ya
kumaliza mkataba wake wa awali mwishoni mwa msimu katika klabu ya bingwa
Tanzania Bara, Simba SC.
Kiongozi
mmoja wa Simba ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba klabu hiyo
imeridhika na huduma ya mchezaji huyo mrefu na inahitaji kuendelea naye.
Kumekuwa na
mawazo tofauti ndani ya Simba SC kuhusu Sunzu, ambaye kwa sasa ndiye mchezaji
anayelipwa mshahara mkubwa zaidi Tanzania, Sh Milioni 5, kwamba hachezi kwa
kiwango cha fedha anazolipwa.
Lakini
wengine wanaamini Sunzu anawajibika vizuri na anastahili kwa fedha anayolipwa.
Pamoja na hayo, hali ya kiuchumi ndani ya klabu hiyo kwa sasa, inatia shaka
kama itaweza kuurudia mkataba ule ule wa Sunzu.
Hata hivyo,
habari zaidi zinasema kwamba Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange
‘Kaburu’ ameamua kumaliza suala la Sunzu kwa kumsainisha mkataba mpya hivi
karibuni.
Baada ya
kumaliza mkataba wa awali, Simba ili kuendelea kuishi na Sunzu, inakadiriwa kumpa
fedha ya dau la usajili, ambalo kwa mwaka haliwezi kuwa chini ya dola za
Kimarekani 15,000 (zaidi ya Sh. Milioni 20 za Tanzania) na kukubaliana kuhusu
mshahara uwe ule ule au mpya.
Kulingana
zengwe lililotawala juu ya dola za Kimarekani 3,500 anazolipwa Sunzu kuna
uwezekano Simba ikataka kuuteremsha mshahara huo, lakini habari zilizopatikana
jana zimesema kwamba Sunzu ataendelea kulipwa mshahara ule ule katika mkataba
wake mpya.
Kumalizika
kwa mkataba wa Sunzu ni mtihani mwingine kwa Simba, ambayo kwa sasa inakabiliwa
na kasheshe la kuingia mkataba mpya na mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi
ambaye yuko vizuri kisoka na anatolewa macho na Azam na Yanga.
Na suala la
usajili linaonekana kuwa zito kwa wakati huu, kwa sababu Kamati ya Utendaji ya
Simba SC wiki hii imevunja Kamati zote ndogondogo, ikiwemo Kamati ya Usajili,
iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Zacharia Hans Poppe.
Hata hivyo,
inadaiwa vibopa wa Kamati ya Usajili, akiwemo Hans Poppe watarejeshewa majukumu
hayo.